Heche Aita Wananchi Kisutu Usikilizwaji Kesi ya Lissu Leo

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetoa wito kwa wananchi wote wapenda haki, demokrasia ya kweli, pamoja na mashirika ya kiraia, Jumuiya za Kimataifa na Kitaifa, kufuatilia kwa karibu na kuhudhuria kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Mheshimiwa Tundu Lissu. Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa kesho, Jumatatu tarehe 2 Juni 2025, katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam kuanzia saa tatu asubuhi.

Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Wegese Heche, kupitia taarifa yake rasmi kwa vyombo vya habari. Heche amesema kesi hiyo si ya kawaida, bali ni tukio muhimu linalogusa msingi wa haki, uhuru wa kisiasa na mustakabali wa utawala wa sheria nchini. Amesema huu ni wakati muhimu kwa wananchi kuonesha mshikamano wao na kusimama kidete kutetea misingi ya demokrasia.

Kwa mujibu wa Heche, kesi hiyo dhidi ya Tundu Lissu ni jaribio la kutishia harakati za kisiasa za kidemokrasia nchini na inaweza kuwa na athari kubwa kwa namna taifa linavyolinda uhuru wa kujieleza, wa kisiasa, na wa kutoa maoni. Amesisitiza kuwa si Tundu Lissu peke yake anayehukumiwa, bali ni dhana nzima ya haki na uhuru wa kisiasa inayopimwa mbele ya macho ya Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa.

Chadema imesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kushiriki kwa amani na utulivu katika kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo, na kuonesha kuwa Watanzania wanajali haki na utawala wa sheria. Viongozi wa chama hicho wamewataka Watanzania kutambua kuwa uamuzi wa kesi hiyo unaweza kuwa na athari pana kwa mustakabali wa siasa za upinzani na maendeleo ya demokrasia nchini.

Kwa kuzingatia umuhimu wa kesi hiyo, chama kimeeleza kuwa ni fursa ya kihistoria kwa Watanzania kuonesha mshikamano na kuwataka wote wenye nafasi kufika mahakamani au kufuatilia kwa njia nyingine yoyote iliyopo kwa lengo la kujifunza, kuhamasika na kuonyesha msimamo wao kwa njia ya amani kuhusu hatma ya haki nchini Tanzania.

Chanzo: JAMBO TV

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *