
Kocha Misri Awaka “Kombe la Dunia 2026 Wamepanga Argentina Awe Bingwa”
Baada ya Mafarao, Misri kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Dunia 2026, Kocha mkuu wa timu hiyo, Hossam Hassan amelalamikia maamuzi ya waamuzi waliochezesha mchezo huo uliomalizika kwa Argentina kufuzu robo fainali akidai mchezo huo ni wizi uliopangwa ili kuibakisha Argentina mashindanoni.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Hossam amesema hatojali matokeo ya kile atakachokisema ila hii ilikuwa mechi ya wizi uliopangwa na kwamba Dunia nzima iliona kwamba maamuzi ya waamuzi yalikuwa upande wa Argentina, akidai michuano hiyo ‘imeelekezwa’ kwa ajili yao.
“Nitasema kilicho akilini mwangu bila kujali matokeo, hii ilikuwa mechi ya wizi uliopangwa na dunia nzima iliona, Na ninataka kusema jambo moja zaidi, kama wanataka Argentina washinde, kwa nini waite kila mtu aje kushiriki?” — amesema mfungaji huyo wa muda wote wa timu ya Taifa ya Misri.
Malalamiko hayo yamatokana na matukio makuu mawili kwenye mchezo huo ambayo ni pamoja na kukataliwa kwa bao la Misri lililofungwa na Zico ambalo lingewapa uongozi wa 2-0 likifutwa na VAR huku akidai wakati matokeo yakiwa 2-2, Argentina walifanya shambulizi la kushtukiza na kupata goli la ushindi la tatu wakati kulikuwa na tukio la madhambi ambalo pengine lingewapa mafarao hao bao la tatu.
