Nature

Lake Oil Watoa Tamko Baada ya Vituo vyake 38 Kuchomwa Moto

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni ya Lake Oil Group, Stephen Mtemi, amekanusha vikali taarifa zinazoenezwa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari kuwa kampuni hiyo inamilikiwa na mwanasiasa maarufu nchini. Ametoa ufafanuzi huo kufuatia uvumi ulioibuka baada ya vituo vya mafuta vya kampuni hiyo kuvamiwa na kuchomwa moto katika matukio yaliyotokea tarehe 29 Oktoba 2025 katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa Mtemi, jumla ya vituo 38 vya mafuta vya Lake Oil viliharibiwa vibaya, hatua iliyosababisha kampuni kupata hasara kubwa na kuathiri ajira za mamia ya wafanyakazi. Amesema kuwa uvumi huo wa kisiasa ndio uliosababisha kundi la watu wenye hasira kuvamia na kuharibu mali kwa madai kwamba wanapambana na wanasiasa wanaodaiwa kumiliki kampuni hiyo.

Watu wengi wanahusisha Lake Oil na mwanasiasa fulani, jambo ambalo si la kweli. Ndiyo sababu tulisikia washambuliaji wakitamka wazi kuwa wanashambulia vituo vyetu kwa kudhani vina uhusiano na wanasiasa,” alisema Mtemi.

Aidha, amefafanua kuwa kampuni ya Lake Oil ni mali halali ya Mtanzania mwenye jina Ally Awadhi, ambaye hana uhusiano wowote wa kisiasa wala kibiashara na wanasiasa wanaotajwa kwenye uvumi huo.

“Tunaomba umma wa Watanzania uelewe kuwa Lake Oil ni kampuni binafsi, inayomilikiwa na Ally Awadhi, na haina uhusiano wowote na wanasiasa. Si kweli kwamba kuna mwanasiasa yeyote anayemiliki au kuwa na hisa katika kampuni yetu,” alisisitiza.

Mtemi ameongeza kuwa kutokana na uharibifu huo, wafanyakazi takribani 300 wamepoteza ajira kwa muda na wamelazimika kupewa likizo ya bila malipo hadi pale matengenezo ya vituo hivyo yatakapokamilika.

Vituo vyote 38 vilivyochomwa vilikuwa na wafanyakazi 300 ambao kwa sasa wapo nje ya kazi. Tumewapa likizo ya muda bila malipo hadi tutakapoweza kurejesha shughuli katika hali ya kawaida,” alisema.

Amehitimisha kwa kuitaka serikali na vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha mashambulizi hayo na kuwachukulia hatua wahusika wote waliopanga na kutekeleza uhalifu huo. Pia ametoa wito kwa wananchi kuacha kusambaza taarifa zisizo sahihi ambazo zinaweza kuharibu taswira ya kampuni na kuathiri uchumi wa taifa.

Related Posts