
MFANYAKAZI wa ndani Neema Justine (19), mkazi wa Kata ya Old Shinyanga Manispaa ya Shinyanga amefariki dunia akidaiwa kujinyonga ndani ya nyumba aliyokuwa akifanya kazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi, amebainisha hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu juu ya tukio hilo.
Amesema, tukio hilo limetokea jana majira ya saa sita mchana wakati mama mwenye nyumba akiwa amekwenda kazini, ndipo mfanyakazi huyo alipokutwa amejinyonga.
“Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, tunaendelea kufanya uchunguzi juu ya kifo cha mfanyakazi huyo, ambaye amekutwa amefariki kwa kujinyonga ndani ya nyumba aliyokuwa akifanya kazi,” amesema Magomi.
Naye, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Soko B, Oldshinyanga Leonardo Magige, amesema kwa mujibu wa maelezo ya familia na mwajiri, siku ya tukio, mama mwenye nyumba baada ya kumaliza kufua nguo, aliondoka kwenda kazini na mtoto wake na kumuacha mfanyakazi peke yake.
“Mama huyo baada ya kurejea nyumbani ndipo alipomkuta mfanyakazi wake akiwa amefariki kwa kujinyonga dirishani na hakuacha ujumbe wowote.
“Baada ya kupata taarifa hizo, niliwasiliana na polisi kata, ambaye alipiga simu polisi na maofisa walifika eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu, na kuupeleka hospitali ya Manispaa ya Shinyanga kwa uchunguzi zaidi,” amesema Magige.
Aidha, katika Kata hiyo ya Oldshinyanga ni tukio la pili sasa kutokea ndani ya wiki mmoja, ambapo Aprili 27 mwanafunzi aliyekuwa akisoma kidato cha nne shule ya Sekondari Olshinyanga Rebeka Maganga (17) alifariki kwa kudaiwa kujinyonga chumbani kwake
