Mtoto wa Muammar Gaddafi Auawa Kwa Risasi….

Saif al-Islam Gaddafi, mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi, ameripotiwa kupigwa risasi na kuuawa.

Kifo cha mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 53, ambaye hapo awali alionekana kuwa mrithi wa baba yake, kilithibitishwa na Shirika la habari la Libya.

Wakili wake aliambia shirika la habari la AFP kwamba kikosi cha “makomandoo wanne” kilifanya mauaji nyumbani kwake katika jiji la Zintan, ingawa haikuwa wazi ni nani aliyehusika na shambulio hilo.

Hata hivyo, dada yake alitoa taarifa zinazokinzana na hizo akiambia televisheni ya Libya kwamba alifariki karibu na mpaka wa nchi hiyo na Algeria.

Saif al-Islam Gaddafi kwa muda mrefu alionekana kama mtu mwenye ushawishi mkubwa na anayeogopwa zaidi nchini baada ya baba yake, ambaye alitawala Libya kuanzia 1969 hadi alipoondolewa madarakani na kuuawa wakati wa uasi mwaka 2011.
Mnamo mwaka wa 2015, alipewa hukumu ya kifo bila kuwepo mahakamani na mahakama ya Libya.

Gaddafi alikuwa akikana kila mara kwamba alitaka kurithi madaraka kutoka kwa baba yake, akisema hatamu za madaraka hazikuwa “shamba la kurithi”.

Hata hivyo, mwaka wa 2021 alitangaza kwamba angegombea urais katika chaguzi ambazo baadaye ziliahirishwa kwa muda usiojulikana.

Related Posts