
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia na linaendelea kumhoji mkazi wa Mtaa wa Temeke kata ya Mhandu, wilaya ya Nyamagana, Loveness Daniel Kisile (30) kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kwa mume wake na ndugu zake akidai ametekwa na watekaji wanahitaji Milioni 10 ili wasimdhuru na kutoa mimba yake.
Akizungumza leo na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbroad Mutafungwa amesema tukio hilo limetokea Septemba 24, 2025 ambapo mtuhumiwa anadaiwa kutenda kosa hilo ili kumdanganya mume wake na wakwe zake waendelee kumuamini na kutoa mahali nyumbani kwao huku fedha akihitaji kwa manufaa yake.
“Mtuhumiwa Loveness Daniel kisile alitoa taarifa ya uongo kwa kumpigia simu mume wake aitwaye Hosea Joel Lusigwa, kwamba ametekwa na watu watatu wa jinsia ya kiume waliokuwa wakitumia usafiri wa pikipiki na gari, ambazo namba zake za usajili hakuweza kuzitambua na akidai watu hao walimkamata kwa nguvu na kumvalisha mfuko wa sulphate usoni kwa lengo la kutowatambua kisha kumpeleka kusikojulikana,” amesema.
Kamanda Mutafungwa amesema baada ya mahojiano ya awali mtuhumiwa alikiri kutoa taarifa za uongo za kutekwa na kutolewa mimba kama alivyokuwa amezitoa awali huku uchunguzi ukibainika kuwa hakuwa na mimba.

