Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemkamata Jenifer Bilikwiza Jovin maarufu kama Niffer (26) mkazi wa Masaki, Kinondoni kwa tuhuma za kuhamasisha vurugu na kuharibu miundombinu katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo, hususan kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Taarifa iliyotolewa Oktoba 27, 2025 na Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro imesema mtuhumiwa alikamatwa majira ya saa 9 mchana katika eneo la Sinza Kumekucha, ambapo alihusishwa na vitendo vya uchochezi vinavyoweza kuhatarisha amani.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam tarehe 27,10.2025 majira ya saa 9 mchana eneo la Sinza Kumekucha limemkamata na linamuhoji Jenifer Bilikwiza Jovin miaka 26 mkazi Masaki Peninsula Kinondoni kwa tuhuma za kuhamasisha vurugu na kuharibu miundombinu katika maeneo mbalimbali jijini hasa siku za kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025”, imesomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Polisi wamesema kuwa hatua zaidi za kisheria zinaendelea kuzingatiwa dhidi ya mtuhumiwa huyo wakati uchunguzi ukiendelea.
Taarifa hiyo imekuja saa chache mchache baada ya kusambaa kwa taarifa za kupotea kwa Niffer huku wengine wakidai kuwa alikuwa ametekwa na watu ambao hawakutambulika mara moja.

