Ikiwa ni siku moja baada ya raia wa Uganda kushiriki katika Uchaguzi Mkuu, vikosi vya usalama nchini humo vimeripotiwa kuzingira makazi ya Kiongozi wa Upinzani na Chama cha National Unity Platform (NUP), Kyagulanyi Ssentamu Robert maarufu kama Bobi Wine, katika hatua inayotafsiriwa kuwa kizuizi cha nyumbani kisicho na uhalali wa kisheria.
Mashuhuda na vyanzo vya NUP wameripoti kuwa askari wa jeshi na polisi waliokuwa na silaha nzito walifunga njia zote zinazoingia na kutoka nyumbani kwake, huku baadhi ya askari wakiruka uzio wa nyumba bila idhini na kuanza kuweka mahema ndani ya eneo la makazi hayo.
Imeelezwa, Kyagulanyi na mke wake walikuwa ndani ya nyumba wakati operesheni hiyo ikitekelezwa bila hati ya kukamatwa, amri ya mahakama, au tamko lolote rasmi kutoka kwa mamlaka husika.
Hatua hiyo imeibua maswali mazito kuhusu uhalali wake kikatiba, hasa ikizingatiwa kuwa inahusisha uvamizi wa faragha, kukiuka haki ya uhuru wa kusafiri, na kuwazuia watu bila msingi wa kisheria. Wanaharakati na wataalamu wa sheria wanaitaja operesheni hiyo kuwa ni ukiukwaji wa haki za msingi.
Vyanzo vya Upinzani vimesema kuwa tukio hilo ni muendelezo wa mbinu za kuwabana viongozi wa upinzani, hasa nyakati za kisiasa zilizo nyeti kama uchaguzi au maandamano
Hali kama hii imewahi kushuhudiwa mara kadhaa nchini Uganda, na mara nyingi imekosolewa vikali na mashirika ya haki za binadamu ndani ya nchi na kimataifa kwa kudhoofisha misingi ya demokrasia na uhuru wa kisiasa.
Hadi sasa, Jeshi la Polisi la Uganda na vyombo vingine vya usalama havijatoa maelezo kuhusu sababu au uhalali wa operesheni hiyo.
Wakati huo huo, wakazi wa eneo la karibu wameripoti kuwepo kwa vizuizi vya barabarani, doria zilizoongezeka na udhibiti mkali wa eneo, hali inayoongeza wasiwasi miongoni mwa wananchi.
Mashirika ya haki za binadamu yanaendelea kushinikiza utolewaji wa taarifa rasmi na kuheshimwa kwa misingi ya sheria na Katiba, huku wakieleza kufuatilia kwa karibu jinsi hali itakavyoendelea.
