Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, in amewafuta kazi wasaidizi wake wawili waandamizi kufuatia kashfa ya kumteua mtu aliyefariki miaka mitano iliyopita kuhudumu katika jopo muhimu la mazungumzo ya uchaguzi.
Uteuzi wa Steward Soroba Budia, aliyekuwa mwanachama wa chama cha upinzani cha United Democratic Party (UDP), ulitangazwa Januari 30, 2026. Hata hivyo, muda mfupi baadaye vyombo vya habari na raia walibaini kuwa Budia alifariki tangu mwaka 2021, jambo lililozua kejeli na maswali mazito kuhusu ufanisi wa ofisi ya rais.
Kwa mujibu wa BBC, waliokumbwa na rungu la Rais ni David Amour Major- Katibu wa Mawasiliano wa Rais, na Valentino Dhel Maluet, Msimamizi wa Ofisi ya Rais.
Kabla ya kufutwa kazi, David Amour alitoa utetezi kuwa ofisi ya rais ilitegemea majina yaliyowasilishwa na “washikadau” na kukiri kuwa uhakiki wa kina haukufanyika, jambo aliloliita kuwa ni “kosa lililotokea kwa bahati mbaya.”
Jopo hilo liliundwa ili kuratibu mazungumzo kuelekea uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Desemba 2026. Hali ya kisiasa nchini humo bado ni tete, huku Makamu wa Rais wa zamani, Riek Machar, akiwa bado chini ya kifungo cha nyumbani akikabiliwa na mashtaka mazito ya uhaini na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
