
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa muda wa wiki moja kwa watu wote waliopora au kutapeli ardhi na mali za wananchi kuzirejesha mara moja, akionya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokaidi agizo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Chalamila amesema kumekuwepo na wimbi kubwa la migogoro ya ardhi linalosababisha malalamiko na kilio kwa wananchi, hali inayohitaji hatua za haraka za Serikali.
“Nimewapa muda mfupi kurejesha mali zote zilizoibiwa kinyemela. Ndani ya wiki moja, kila aliyehusika ahakikishe anarudisha mali hizo,” amesema.
Ameeleza kuwa kufuatia ziara alizozifanya katika baadhi ya maeneo ya jiji, tayari zaidi ya maeneo 16 yamerudishwa kwa siri na wahusika, na Serikali imeamua kuwasamehe waliorejesha mali hizo kwa hiari bila kushinikizwa.
Maeneo Yanayoongoza kwa Migogoro
Chalamila ametaja maeneo yanayoongoza kwa malalamiko ya utapeli wa ardhi kuwa ni Kigamboni, Ilala na sehemu nyingine za jiji. Amesema ofisi yake imepokea malalamiko mengi yanayohusu uporaji wa viwanja, ubadilishaji holela wa umiliki pamoja na mikataba kandamizi ya mikopo inayosababisha wananchi kupoteza mali zao.
Katika hatua nyingine, amefichua kuwepo kwa vitendo vya utapeli katika baadhi ya showroom za magari, ambapo wananchi hulipa fedha nyingi lakini hawakabidhiwi magari yao. Baadhi ya waathirika wanadaiwa kupoteza zaidi ya Sh milioni 100.
Pia ameonya juu ya mikopo umiza, akieleza kuwa baadhi ya wananchi husainishwa mikataba ya kuuza mali zao wanapochukua mikopo, na baadaye kujikuta wamepoteza maeneo yao bila matarajio.
Chalamila amesema kuanzia Machi 9 ataanza ziara ya kukagua maeneo yaliyoathirika ili kusikiliza kero za wananchi moja kwa moja na kuhakikisha haki inapatikana.
Amewataka wote waliopatwa na madhara kuwasilisha taarifa zao ofisini kwake ili ziweze kufanyiwa kazi haraka, akitoa namba maalum ya kupokea malalamiko 0733 206 952. Amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo vya unyang’anyi na itaendelea kulinda mali za wananchi kwa mujibu wa sheria.
