Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Senegal imetwaa ubingwa wa Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Morocco katika mchezo wa fainali uliochezwa usiku wa Januari 18, 2026 nchini Morocco.
Mchezo huo ulikuwa wa ushindani mkubwa huku timu zote zikionesha kiwango cha juu, jambo lililosababisha dakika 90 za kawaida kumalizika bila mshindi na kulazimika kuongezwa dakika 30 za muda wa nyongeza.
Dakika ya 107 ya mchezo huo, mshambuliaji wa Senegal Pape Alassane Gueye alipachika bao la pekee lililoihakikishia Senegal ushindi na hatimaye kutwaa taji la AFCON kwa mara ya pili katika historia ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Mshindi wa kwanza AFCON 2025 Senegal amepewa zawadi ya Dola za Kimarekani Milioni 10 (takriban Shilingi Bilioni 24.7 za Kitanzania), ongezeko kubwa kutoka 2023.
Mshindi wa pili Morocco amepokea Dola Milioni 4, kama ilivyotangazwa na Rais wa CAF Patrice Motsepe, kwa ajili ya kuongeza motisha na ushindani kwenye fainali hizo.
Morocco imepoteza fainali ya pili baada ya kupoteza ile ya mwaka 2004 dhidi ya Tunisia.
