Mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama cMapinduzi (CCM) wa kumpata mgombea wa Umeya wa Jiji la Dar es Salaam umeingia katika sura mpya baada ya matokeo yake kuibua mshangao mkubwa na kubadili taswira ya matarajio ya awali.
Katika uchaguzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa CCM Wilaya ya Ilala, Diwani wa Mchikichini, Nurdin Juma (Shetta), ameibuka mshindi baada ya kupata kura 25, akimshinda Diwani wa Kata ya Segerea, Robert Manangwa, aliyepata kura 21.
Ushindi huo umefikiwa baada ya mchakato wa kura kurudiwa kwa mara ya pili kufuatia duru ya awali kufutwa kutokana na mgombea aliyekuwa anaongoza kushindwa kufikisha nusu ya kura halali 52 zilizopigwa.
Hatua hiyo iliyowashangaza wengi, kwani aliyekuwa anatetea nafasi hiyo na ambaye alionekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda, Omary Kumbilamoto, kuondolewa mapema baada ya kupata kura nne tu katika duru ya kwanza.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchakato huo, Msimamizi wa uchaguzi huo, Haji Kilimo ambaye ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM, amethibitisha kuwa mshindi amepatikana kwa mujibu wa taratibu baada ya mchakato wa kura kurudiwaa
Ili kumpata mshindi katika duru ya pili, Kumbilamoto na Saad Khimji waliondolewa kwenye mbio hizo, na nafasi kupewa Shetta na Manangwa ambao kura zao zilikuwa zimekaribiana zaidi.

