
Jeshi la Polisi Tanzania limesema linawafuatilia kwa karibu baadhi ya watu wanaohamasisha kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu pamoja na kusambaza matamshi na jumbe zao mitandaoni kwa lengo la kuleta taharuki kwa jamii.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, DCP David Misime, amesema leo Jumapili Februari 22, 2026 kuwa ufuatiliaji huo unafanyika usiku na mchana, huku akiwataka wananchi kutokuwa na hofu na kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii kama kawaida.
Polisi imewataka wananchi kuwapuuza watu hao pamoja na taarifa na jumbe wanazosambaza, ikibainisha kuwa hawapo ndani ya mipaka ya Tanzania na hata wanachokihamasisha hawatashiriki nacho wala hawatakuwa na uwezo wa kushiriki.
“Wananchi watambue lengo la watu hao ni kutaka kutuchonganisha, kutujengea chuki ili tuhamasike kujiingiza kwenye uhalifu na vitendo vya vurugu. Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua yeyote yule atakayeendelea kujihusisha na vitendo kama hivyo au kujiingiza katika uhalifu wa aina yoyote ile kwani ni kinyume cha sheria,”
amesema Kamanda Misime.
Polisi pia imemtaja mmoja wa watu wanaoshawishi uhalifu kuwa ni anayejitambulisha kwa jina la TFF, ambaye amekuwa akitoa taarifa mbalimbali ikiwemo kudai kufanya mazoezi porini na kutekeleza matukio ya kijinai, madai ambayo Polisi imeyakanusha na kusema taarifa zake zote ni za uongo.
