Refa wa mchezo wa hatua ya kufuzu robo fainali kati ya Morocco na Tanzania amejikuta kwenye lawama kali kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka, baada ya kudaiwa kushindwa kutafsiri vyema sheria za mchezo huo.
Baadhi ya Watanzania wamesema Taifa Stars walinyimwa penati ya wazi kipindi cha pili cha mchezo huo, baada ya mchezaji wa Morocco kudaiwa kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari. Licha ya malalamiko kutoka kwa wachezaji wa Tanzania, refa aliendelea na mchezo bila hata kwenda kuangalia teknolojia ya VAR, jambo lililozua mjadala mkubwa uwanjani na mitandaoni.
Mashabiki wengi wameeleza kushangazwa na uamuzi huo, wakidai VAR ilipaswa kutumika ili kutoa haki kwa pande zote mbili, hasa ikizingatiwa umuhimu wa mchezo huo wa hatua ya mtoano.
Hata hivyo, Morocco waliendelea kusonga mbele huku Tanzania ikimaliza safari yake kwenye michuano hiyo, jambo lililoacha maswali mengi kuhusu maamuzi ya waamuzi na matumizi sahihi ya VAR kwenye michezo mikubwa ya kimataifa.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) bado halijatoa tamko rasmi kuhusu tukio hilo, wakati mashabiki wakiendelea kudai haki na uwazi zaidi katika usimamizi wa mechi za ngazi ya juu barani Afrika.
