Twiga Stars, yashindwa kutinga robo fainali WAFCON

Ndoto za Twiga Stars kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 zimezimika baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Ivory Coast katika mchezo wa mwisho wa Kundi B uliochezwa usiku wa kuamkia leo kwenye Uwanja wa Larbi Zaouli, Casablanca nchini Morocco.

Ushindi huo umeifanya Ivory Coast kumaliza kileleni mwa Kundi B ikiwa na pointi saba baada ya kushinda mechi mbili na kutoka sare moja, huku Twiga Stars ikimaliza katika nafasi ya tatu na pointi tatu, hivyo kuaga rasmi mashindano hayo.

Ivory Coast ilianza kuonyesha makali yake mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya Nsira Ouedraogo kufunga bao la kuongoza dakika ya 44 akimalizia pasi safi ya Ines Konan, na kuipeleka timu yake mapumzikoni ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili, Ivory Coast iliendelea kutawala mchezo na kuongeza bao la pili dakika ya 68 kupitia Ines Konan, aliyefunga kwa mkwaju wa penalti baada ya mwamuzi kuamuru adhabu hiyo.

Twiga Stars ilijaribu kurejea mchezoni kwa kushambulia mara kadhaa, lakini ilikumbana na ukuta imara wa safu ya ulinzi ya Ivory Coast, iliyodhibiti vyema mashambulizi ya Tanzania.

Dakika ya tisa ya muda wa nyongeza, Tanzania ilipata penalti iliyotumbukizwa wavuni na Diana Msewa, lakini bao hilo la kufutia machozi halikutosha kuizuia Twiga Stars kuondoshwa kwenye michuano hiyo.

Katika mchezo mwingine wa Kundi B, mabingwa watetezi Afrika Kusini waliifunga Burkina Faso bao 1-0 na kutinga robo fainali wakiwa washika nafasi ya pili nyuma ya Ivory Coast.

Licha ya kuaga mashindano, Twiga Stars imeandika historia kwa kupata ushindi wake wa kwanza kabisa katika fainali za WAFCON, baada ya kuifunga Afrika Kusini kwenye mchezo wa pili wa hatua ya makundi.

Pia, Tanzania imeonyesha maendeleo kwa kufanikiwa kufunga angalau bao moja katika kila mchezo wa hatua ya makundi, ingawa juhudi hizo hazikutosha kuipeleka kwenye hatua ya mtoano.

Related Posts