
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, leo Alhamisi Mei 28, 2026 imeifuta rasmi hati ya kesi ya madai iliyokuwa imefunguliwa dhidi ya uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), hatua inayohitimisha kwa sasa shauri hilo lililokuwa likifuatiliwa kwa karibu na wadau wa siasa nchini.
Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Saidi Issa Mohamed pamoja na wenzake, ambao walikuwa wakidai kuwepo kwa mgawanyo usio sawa wa mali na rasilimali za chama kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Shauri hilo lilikuwa limefunguliwa dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Chadema pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Akitoa uamuzi huo, Jaji D. Ngunyale amesema mahakama imekubali pingamizi la awali lililowasilishwa na upande wa utetezi wa Chadema, baada ya kubaini kuwa hati ya madai ilikuwa na mapungufu ya kisheria ambayo yameondoa uwezo wa mahakama kusikiliza shauri hilo.
Kwa mujibu wa uamuzi huo, mahakama imesema haikuweza kujiridhisha kama ina mamlaka ya kisheria kuendelea kusikiliza kesi hiyo, hivyo imeamua kuifuta hati hiyo ya madai kutokana na mapungufu yaliyoainishwa.
Uamuzi huo unaweka mwisho wa hatua ya awali ya kesi hiyo, huku upande wa Chadema ukitoka na ushindi katika pingamizi hilo la kisheria.
