Nature

Waliochaguliwa Kujiunga Kidato Cha Kwanza Mwaka 2026

Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),Prof. Riziki Shemdoe akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo,kuhusu wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2026. Picha na Michael Matemanga
Dar es Salaam. Wanafunzi 937,581 sawa na asilimia 100 ya wanafunzi wote waliokuwa na sifa wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2026 na kupangiwa shule.

Wanafunzi hawa ni wale waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka, 2025 na kupata jumla ya alama za ufaulu kati ya 121 hadi 300.

Shule hizi zinapangwa wakati ambao wazazi wakitakiwa kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanaripoti shuleni na kubaki shuleni hadi wanapohitimu kidato cha nne.

Hayo yameelezwa leo Desemba 4, 2025 na Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe apokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya uchaguzi huo wa wanafunzi.

Profesa Shemdoe amesema uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo wa 2026 umefanyika kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

”Kila Mtahiniwa aliyefanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka, 2025 na kupata jumla ya alama za ufaulu kati ya 121 hadi 300 amechaguliwa na kupangiwa shule ya Serikali,” amesema.

Amesema uchaguzi huo umehusisha wanafunzi 937,581 sawa na asilimia 100 ya wanafunzi wote waliokuwa na sifa ya kuchaguliwa wakiwemo wasichana 508,477 na wavulana 429,104.

“Jumla ya wanafunzi 937,581 wakiwemo wasichana 508,477 na wavulana 429,104 ikijumuisha wanafunzi wenye Mahitaji Maalum 3,228 wakiwemo wasichana 1,544 na wavulana 1,684 wamepangwa katika shule za sekondari za Serikali 5,230 kwa ajili ya kuanza masomo ya Kidato cha Kwanza mwaka, 2026,” amesema.

Amesema wanafunzi 815 wamechaguliwa kujiunga katika shule za eenye ufaulu wa alama za juu wakiwemo wasichana 335 na wavulana 480.

“Hao wamechaguliwa kwenye shule za sekondari ambazo hupokea wanafunzi wenye ufaulu wa alama za juu kama Ilboru, Msalato, Kibaha, Kilakala, Mzumbe, Tabora Boys na Tabora Girls,” amesema.

Wanafunzi 3,411 wamechaguliwa shule za amali za bweni wakiwemo wasichana 1,279 na wavulana 2,162.

Pia wanafunzi 7,360 wamechaguliwa kujiunga na shule za bweni za kitaifa wakiwemo wasichana 5,014 na wavulana 2,346.

“Pia wanafunzi 925,065 wamechaguliwa kujiunga shule za sekondari za kutwa

na kati yake wasichana ni 501,849 na wavulana 424,116. Hizi ni shule za sekondari za Kutwa ambazo hupokea wanafunzi kutoka katika eneo la karibu na shule ya msingi aliyosoma mwanafunzi husika,” amesema.

Profesa Shemdoe amesema Serikali ilifanya maandalizi mapema ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote watakaofaulu mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka, 2025 wanajiunga na elimu ya sekondari ifikapo Januari, 2026.

Kutokana na maandalizi hayo wanafunzi wote waliochaguliwa wataanza muhula wa kwanza wa masomo wa mwaka 2026 utakaoanza tarehe 13 Januari, 2026.

“Napenda kuwaasa wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2026 nchini watumie vizuri fursa waliyoipata kusoma kwa bidii ili wafikie malengo waliojiwekea na matarajio ya wazazi,” amesema Profesa Shemdoe.

Profesa Shemdoe aliitaka Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinahimizwa kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa mitaala mipya ambayo ilianza kutumika Januari, mwaka 2024.

“Katika uwezeshaji mtaala huo ninaagiza Kila shule ya sekondari itumie vema kipindi cha maandalizi (orientation) kwa wanafunzi kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuwasiliana katika lugha ya Kiingereza na kuchagua aina ya fani wanazopenda kusoma katika shule zenye mkondo wa amali zisizo za kihandishi;,” amesema.

Pia, aliwataka wazazi au walezi kufanya maandalizi ya kutosha kwa watoto waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka wa masomo 2026 ili kuepuka watoto kuchelewa kuanza masomo yao kwa wakati.

Kwa upande wa halmashauri aliagiza Mikoa na Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha kwanza mwaka wa masomo 2026 wanaripoti shuleni na kuandikishwa ili kupata haki yao ya msingi ya elimu.

“Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, viongozi na watendaji wa halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa elimu kuhakikisha Wanafunzi wanaanza masomo yao Januari, 2026 bila vikwazo vya aina yoyote ili kutekeleza azma ya Serikali ya utoaji wa elimumsingi bila malipo,” amesema.

Ili kufanikisha hilo aliwataka Wakuu wa Mikoa, makatibu tawala wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa shule kuhakikisha maandalizi yote kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka, 2026 yanakamilika kwa wakati.

“Pia ninawahimiza wazazi, walezi na jamii kushirikiana na uongozi wa shule, mikoa, wilaya na halmashauri ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliochaguliwa wanaandikishwa, wanahudhuria na kubakia shuleni hadi watakapohitimu elimu ya sekondari,” amesema.

Related Posts