
Baraza la Mitihani la Tanzania () limefuta matokeo ya watahiniwa 58 baada ya kubainika kujihusisha na udanganyifu katika mitihani ya kitaifa, ikiwemo matumizi ya njia zisizoruhusiwa wakati wa kufanya mitihani.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Baraza hilo, kati ya watahiniwa waliofutiwa matokeo, 44 ni wa Mtihani wa Kidato cha Sita, huku 14 wakiwa wa Mtihani wa Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Msingi (DPEE). Taarifa hiyo imeeleza kuwa baadhi ya watahiniwa hao walibainika kutumia zana za kisasa za kidijitali, ikiwemo programu za akili unde (AI) kama , katika kujaribu kufanya udanganyifu wa mitihani.
NECTA imesisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kudhibiti viwango vya uadilifu katika mitihani ya kitaifa na kuhakikisha kuwa sifa za kitaaluma zinapatikana kwa haki na uwazi.
Katika hatua nyingine, Baraza hilo pia limechukua uamuzi wa kukifungia kituo cha mitihani cha P5584 Excellency Open School kilichopo mkoani Manyara, kufuatia kubainika kukiuka miongozo na taratibu za uendeshaji wa mitihani ya taifa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kituo hicho kitaendelea kufungwa hadi pale NECTA itakapofanya tathmini na kujiridhisha kuwa kinakidhi vigezo na viwango vinavyotakiwa ili kuendesha mitihani kwa usalama na uadilifu.
Hatua hizo zimekuja katika kipindi ambacho mamlaka za elimu nchini zinaongeza juhudi za kudhibiti udanganyifu wa mitihani unaosababishwa na matumizi ya teknolojia za kisasa pamoja na mbinu nyingine zisizoruhusiwa.
NECTA imetoa wito kwa wanafunzi, walimu na wadau wote wa elimu kuzingatia maadili ya mitihani na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha mustakabali wa elimu nchini.
