
POLISI wa Uganda wamewakamata wanawake wawili, wote wakiwa katika umri wa miaka 20, baada ya majirani kuripoti kuwaona wakibusiana hadharani, kitendo ambacho kimeharamishwa chini ya Sheria ya Kupinga Mapenzi ya Jinsia Moja nchini humo.
Katika taarifa iliyotolewa jana na Jeshi la Polisi nchini humo, walisema wawili hao walikamatwa huko Arua, kaskazini magharibi mwa Uganda, na kwamba majirani waliwapiga picha kabla ya kuwaarifu polisi.
Pia ilielezwa kuwa wanawake hao wanaendelea kuzuiliwa bila kupata uwakilishi wa kisheria.
Sheria ya nchi hiyo inatoa adhabu kali, ikiwa ni pamoja na kifungo cha maisha jela na hukumu ya kifo kwa mahusiano ya jinsia moja, na kwamba adhabu hizo ziliwekwa kwasababu idadi ya kesi za aina hiyo zimezidi kiwango.
Polisi waliarifiwa na majirani waliosema wawili hao walikuwa wamejihusisha na tabia ya mapenzi ya jinsia moja, AFP inaripoti.
“Majirani waliwasiliana na polisi wakilalamika kwamba wawili hao walikuwa wakifanya mapenzi ya jinsia moja na walionekana wakibusiana hadharani,” msemaji wa polisi wa eneo hilo Josephine Angucia alisema.
Aliongeza kuwa majirani walitoa picha walizodai zilionyesha wawili hao wakibusiana hadharani.
Angucia aliongeza kuwa wakazi pia waliripoti kuona makundi ya wanawake wakitembelea nyumba ya wawili hao yenye chumba kimoja cha kulala na kulala usiku kucha, jambo ambalo waliamini liliashiria mikusanyiko ya watu wa jinsia moja.
Alisema kesi hiyo imefikishwa kwa waendesha mashtaka kwa ajili ya mapitio na uwezekano wa kuwasilishwa mahakamani.
Sheria ya Uganda ya Kupinga Mapenzi ya Jinsia Moja ni miongoni mwa sheria kali zaidi duniani.
Watu waliopatikana na hatia wanakabiliwa na kifungo cha maisha jela kwa mahusiano ya kimapenzi ya jinsia moja.
Pia ilielezwa kuwa wale waliopatikana na hatia ya kesi zilizopitiliza, ikiwa ni pamoja na makosa ya kurudia kitendo hicho au vitendo vinavyowahusisha watoto au watu walio katika hatari wakikabiliwa na adhabu ya kifo.
Sheria hiyo imeshutumiwa na serikali za Magharibi na makundi ya kutetea haki za binadamu.
Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu Frank Mugisha alikosoa kukamatwa huko katika maoni yaliyochapishwa kwenye mtandao wa X, akisema kunaangazia mazingira hatari ambayo Waganda wa jamii ya LGBTQ+ wanakabiliana nayo.
Alionya kwamba sheria hiyo imesababisha ulaghai, huku waathiriwa mara nyingi wakiogopa sana kushtakiwa kiasi cha kutoweza kutafuta msaada.
Uganda ni taifa lenye wahafidhina wengi na idadi kubwa ya raia ni Wakristo.
Imekabiliwa na uchunguzi mkali wa kimataifa tangu sheria hiyo ilipoanza kutekelezwa mnamo mwezi Mei 2023.
Umoja wa Mataifa (UN) na serikali kadhaa za kigeni zimelaani sheria hiyo.
Benki ya Dunia ilisitisha kwa muda mikopo kwa Uganda kabla ya kuirejesha mwaka wa 2025
