
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, amesema haiwezekani kila sheria inapokiukwa, wahusika kudai busara au maridhiano, akisisitiza kuwa sheria lazima zifuatwe.
Wasira amesema maridhiano yapo, lakini hayapaswi kutumika kama mbadala wa sheria, akieleza kuwa suala la Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, linaendelea Mahakamani kwa kufuata taratibu za kisheria baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kufungua kesi dhidi yake.
“Yapo maridhiano na zipo sheria, si vizuri tukazoea kuwa wewe ukiivunja sheria jibu lake liwe maridhiano. Zipo njia na Tundu Lissu yupo Mahakamani kwa kufuata taratibu za kisheria,” amesema Wasira.
Amesema Majaji wameeleza kuwa wanakusudia kuendesha shauri hilo mfululizo kwa siku 20, huku akisisitiza kuwa Mahakama ndiyo yenye jukumu la kuamua hatima ya kesi hiyo.
Wasira pia amegusia suala la busara lililotumika katika kesi ya Freeman Mbowe, akisema hatua hiyo haipaswi kutafsiriwa kuwa kila anayekiuka sheria anapaswa kupewa busara.
“Haiwezekani kila mkivunja sheria ndio mnahitaji busara. Busara pia lazima iwe pande zote mbili. Kwa Mbowe ilikuwa ni busara ili wajifunze, sasa hawajifunzi, wanaendelea tu kukosea,” amesema.
Ameongeza kuwa Tundu Lissu anapata nafasi ya kujitetea Mahakamani, na iwapo ushahidi hautatosheleza ataachiwa, lakini ukitosheleza Mahakama inaweza kumtia hatiani na kumpa adhabu kwa mujibu wa sheria
