Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura kuondoa tamko la kumtafuta Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na badala yake wamwache ajitokeze aendelee na ibada zake ili wajenge umoja wa kitaifa.
Hatua hiyo inakuja siku saba baada ya Dkt. Mwigulu kuagiza kufunguliwa kwa kanisa hilo, Novemba 24, 2025 ambapo alielekeza lipewe miezi sita ya uangalizi kuhusu kuzingatia miiko, masharti na sheria za uendeshwaji wake.
Agizo hilo la Serikali la kufunguliwa kwa kanisa hilo, lilikuja ikiwa zimepita siku 175 tangu Juni 2, 2025 ilipotangaza kufuta usajili wa kanisa hilo kwa kile ilichoeleza limekiuka masharti ya sheria, kwa madai ya kujihusisha na masuala ya siasa.
Dkt. Mwigulu ametoa maagizo hayo leo Jumapili Novemba 30, 2025 alipozungumza katika mkutano wa hadhara viwanja vya Magufuli, Leganga wilayani Arumeru, baada ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na vurugu za Oktoba 29, 2025.
Amesema ibada ni ushirika kati ya Mungu na wanadamu na kuwa kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alisamehe vijana ambao walionekana wamepita kwenye mkumbo bila kujua kilichofanyika, akaelekeza msamaha na kwenye taasisi za kidini.

