Utata Waibuka Mahakamani Baada ya Shahidi Kukiri Alikuwa Mtuhumiwa Kabla ya Kuwa Shahidi

Mahakama Kuu imeendelea leo na usikilizwaji wa kesi ya uhaini inayomkabili mwanasiasa wa upinzani, Tundu Lissu, ambapo mshitakiwa aliendelea kumfanyia maswali ya mseto (cross-examination) shahidi wa kificho anayejulikana kama P6.

Katika hatua ya awali, Mhe. Lissu alielekeza maswali yake kwenye maelezo ya awali ya shahidi, akirejea kumbukumbu zilizoandikwa kuhusu ziara ya Mwenyekiti wa CHADEMA wilayani Songea tarehe 6 Aprili 2025. Shahidi alithibitisha kuwepo kwa taarifa hiyo, ingawa baadhi ya majibu yake yalionekana kuwa ya kusita au yenye utata.

Mshitakiwa aliendelea kumkabili shahidi kwa kumrejesha kwenye maelezo yanayodaiwa kutolewa tarehe 10 Aprili 2025, yakihusu mkusanyiko katika uwanja wa Shule ya Msingi Matalawe. Katika maelezo hayo, kulitajwa ujio wa gari la polisi na madai ya kutawanywa kwa mkutano. Hata hivyo, P6 alikana kwamba kauli hizo zipo kwenye maelezo yake rasmi, akisisitiza kuwa taarifa ya kutawanywa au kupigwa mabomu haimo kwenye tamko lake.

Maswali yaliendelea kuhusu tukio la kwenda ofisi za chama eneo la Mfaranyaki, ambapo viongozi walidaiwa kutaka kuzungumza na waandishi wa habari kabla ya polisi kufika. Shahidi alikana pia kuwepo kwa madai ya kupigwa mabomu katika maelezo yake, akisisitiza kuwa hayapo kwenye kumbukumbu zake.

Baada ya kupitia maudhui hayo, Mhe. Lissu alihamisha mwelekeo wa maswali yake kuelekea ufahamu wa shahidi kuhusu sheria. Alimuuliza iwapo, kwa uelewa wake, kauli ya kisiasa kama “bila mabadiliko hakuna uchaguzi” ni kosa la jinai. Shahidi alijibu mara kadhaa kuwa hafahamu. Alipoulizwa iwapo kuzuia uchaguzi ni kosa la jinai au kama kuna sheria inayokataza kufanya hivyo, P6 aliendelea kueleza kuwa hana ufahamu wa masuala ya kisheria.

Mshitakiwa aliendelea kuhoji iwapo polisi walimweleza kuwa matamshi hayo si kosa la jinai au kama walimfundisha nini cha kusema mahakamani. Shahidi hakutoa jibu la moja kwa moja katika swali hilo. Aidha, alipoulizwa kuhusu haki ya kisheria ya vyama kufanya mikutano na iwapo polisi wana mamlaka ya kuzuia mikutano, shahidi alijibu tena kuwa hafahamu.

Katika hatua nyingine, P6 alikiri kuwa alikamatwa tarehe 20 Aprili 2025 katika eneo la DS Kitimoto kwa tuhuma za kufanya maandamano yasiyo ya hiari. Alisema walipelekwa mahakamani na kwamba ndugu yake ndiye aliyekuwa anamsimamia katika mchakato huo wa kisheria. Alipoulizwa kwa nini alibadilika kutoka mtuhumiwa wa kupanga maandamano hadi kuwa shahidi katika kesi ya sasa, shahidi alijibu kuwa hata yeye hafahamu kilichosababisha mabadiliko hayo.

Mhe. Lissu alimuuliza moja kwa moja iwapo aliahidiwa kufutiwa mashtaka kwa masharti ya kuwa shahidi wa upande wa mashtaka. P6 alikanusha madai hayo.

Katika sehemu ya mwisho ya maswali, shahidi alikiri kuwa ni mwanachama wa CHADEMA. Hata hivyo, alipoulizwa ataje tarehe na mwezi alipojiunga rasmi na chama, Wakili wa Serikali Katuga aliingilia kati na kuwasilisha hoja kwamba kujibu swali hilo kunaweza kuhatarisha usiri wa utambulisho wa shahidi, kwani mfumo wa usajili wa chama unaweza kumtambua mtu aliyesajiliwa kwa tarehe husika.

Jopo la majaji lilijadiliana kwa takriban dakika tano kuhusu hoja hiyo kabla ya kutoa mwongozo. Wakati huo, ukumbi wa mahakama ulitulia ukisubiri uamuzi wa majaji kuhusu iwapo swali hilo linaruhusiwa au la, kwa kuzingatia hadhi ya shahidi kama shahidi wa kificho.

Kesi hiyo inaendelea kushika sura ya mijadala ya kisheria kuhusu uhuru wa kisiasa, mamlaka ya vyombo vya dola na uzito wa ushahidi unaowasilishwa. Usikilizwaji unaendelea huku pande zote zikionekana kutumia kila fursa ya kisheria kuimarisha hoja zao mbele ya mahakama.

Related Posts