
Mchambuzi nguli wa soka nchini, Edo Kumwembe, ametoa tathmini yake kuhusu kiwango cha kiungo wa Simba SC, Clatous Chota Chama, katika mchezo wa dabi dhidi ya Yanga uliopigwa hivi karibuni. Katika uchambuzi wake, Kumwembe amebainisha kuwa ingawa Simba walionyesha uhai kupitia kwa Inno Loemba, hali imekuwa tofauti kwa upande wa Chama ambaye amekuwa mhimili wa timu hiyo kwa miaka mingi.
Katika andiko lake, Edo Kumwembe ameeleza upungufu huo wa kiwango cha Chama kama ifuatavyo:
”Katikati ya uwanja Inno Loemba alionekana kuwapa Simba uhai huku akicheza sambamba na kaka yake, Clatous Chotta Chama. Hata hivyo ni wazi miguu imeanza kumsaliti Clatous. Alikuwa anapoteza mipira ovyo. Alikuwa anazidiwa kasi na Damaro. Hakuonekana kuwa na nguvu au ubora wa kuamua mechi kama alivyokuwa anafanya miaka michache iliyopita.”
Maoni haya ya “Legend” yanakuja wakati klabu zote mbili zikiendelea kurushiana maneno ya kejeli, huku Meneja wa Habari wa Simba, Ahmed Ally, akidai kuwa Yanga walikuwa na bahati ya kukwepa kipigo. Kwa upande mwingine, Afisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amewatuhumu Simba kutumia mbinu za nje ya uwanja na ushirikina ili kulazimisha sare hiyo ya bila kufungana
