Polisi Pwani Kuhusu Bawacha “Walikuwa Wanaenda Kutekeleza Uhalifu”

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limetoa ufafanuzi kuhusu kukamatwa kwa wanachama 29 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wakiwemo wanawake 20 na wanaume 9, ambao baadaye waliruhusiwa kwa dhamana.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi iliyotolewa Machi 8, 2026 na Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, wanachama hao walikamatwa Machi 6, 2026 majira ya saa 11 jioni katika eneo la Visiga, wilayani Kibaha, wakiwa wanasafiri kwa kutumia magari mawili aina ya coaster.

Polisi wamesema kukamatwa kwao kulitokana na tuhuma za kukiuka amri ya mahakama pamoja na taarifa za mipango ya kutekeleza vitendo vya kihalifu kwa kisingizio cha kwenda kuazimisha Siku ya Wanawake Duniani mkoani Mara.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanachama hao kwa sasa wapo nje kwa dhamana huku uchunguzi ukiendelea na hatua zaidi za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limewataka wananchi kuendelea kutii sheria, kanuni na taratibu za nchi ili kudumisha amani na utulivu

Related Posts