
Hali ilivyo katika eneo la Mkuyuni Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza baada ya mvua kubwa ambayo imenyesha leo Machi 10, 2026 kwa takribani saa 8 tangu saa 10 alfajiri mpaka saa 7 mchana na kusababisha mafuriko na baadhi ya barabara kushindwa kupitika.
Picha: Damian Masyenene
Hali ilivyo katika eneo la Mkuyuni Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza baada ya mvua kubwa ambayo imenyesha leo Machi 10, 2026 kwa takribani saa 8 tangu saa 10 alfajiri mpaka saa 7 mchana na kusababisha mafuriko na baadhi ya barabara kushindwa kupitika.
Mvua kubwa iliyonyesha katika maeneo mbalimbali ya Mwanza leo Machi 10, 2026 imesababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara, hususan madereva na abiria wa usafiri wa umma.
Mvua hiyo iliyoanza kunyesha majira ya saa 10 alfajiri hadi saa saba mchana imesababisha changamoto kubwa kwa wakazi wa jiji hilo, huku baadhi ya barabara zikifurika maji na kuathiri shughuli za usafiri.
Miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi ni Kata ya Mkuyuni, hasa katika eneo la daraja la Mkuyuni ambalo lilianza kutumika hivi karibuni baada ya kufanyiwa maboresho makubwa yaliyodumu kwa takribani mwaka mmoja.
Kutokana na mvua hiyo, daraja hilo limejaa maji na kusababisha kukatika kwa mawasiliano katika Barabara Kuu ya Kenyatta inayounganisha Mwanza na Misungwi. Hali hiyo imewazuia wakazi wanaosafiri kutoka katikati ya jiji kwenda maeneo ya Nyegezi na Buhongwa kuvuka upande wa pili wa barabara.
Kutokana na hali hiyo, magari ya abiria maarufu kama daladala yanayotoa huduma katika ruti za Nyegezi, Buhongwa na Nyashishi yamelazimika kusitisha safari zao na kuishia katika eneo la Igogo. Abiria wengi wamelazimika kutembea kwa miguu kufika katika maeneo yao.
Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa hali hiyo imeleta usumbufu mkubwa. Mmoja wa abiria, Leopold Anold, amesema amelazimika kutembea kutoka katikati ya jiji hadi Nyegezi kutokana na daladala kushindwa kupita katika daraja la Mkuyuni lililofurika maji.
Naye Felista Michael amesema mvua hiyo imeleta mateso kwa wananchi wengi, akieleza kuwa hali kama hiyo haijashuhudiwa kwa muda mrefu katika jiji hilo.
