
Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu, amemuagiza Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, kukutana na Kamati ya Bunge ya Nishati ili kutathmini hali na mwenendo wa kupanda kwa bei ya mafuta nchini.
Zungu amesema kupanda kwa bei ya mafuta kunaweza kuathiri mipango ya maendeleo ya taifa, akisisitiza kuwa bila nishati hiyo, utekelezaji wa shughuli mbalimbali unaweza kukwama.
Hatua hiyo inakuja kufuatia tangazo la EWURA la bei elekezi mpya za petroli, dizeli na mafuta ya taa zilizoanza kutumika rasmi Aprili Mosi, 2026, ikiwa ni sehemu ya marekebisho ya kila mwezi yanayozingatia mwenendo wa soko la dunia.
Spika Zungu ameeleza kuwa Serikali itatoa taarifa rasmi kuhusu hali ya bei ya mafuta baada ya kamati hiyo kukutana na kufanya tathmini ya kina.
Kwa mujibu wa EWURA, ongezeko hilo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati unaohusisha Iran, pamoja na mashambulizi katika miundombinu ya mafuta ikiwemo visima, maghala na viwanda vya kusafisha mafuta.
Aidha, kufungwa kwa Strait of Hormuz, njia muhimu inayopitisha takriban asilimia 20 ya mafuta duniani, kumeelezwa kuwa kumeongeza gharama za uagizaji wa mafuta nchini.
Kutokana na mabadiliko hayo, bei ya petroli jijini Dar es Salaam imepanda kwa sh. 956 na kufikia sh. 3,820 kwa lita, huku dizeli ikiuzwa kwa sh. 3,806 na mafuta ya taa sh. 3,684, hali iliyozua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi
