
Baada ya makubaliano ya kusitisha vita kwa wiki mbili, Iran imeridhia kufungua Mlango Bahari wa Hormuz ili kuruhusu Meli za kusafirisha mafuta kupita kwenye njia hiyo muhimu ya kimataifa, kimeripoti Kituo cha Televisheni cha Al Jazeera.
Uamuzi wa kufungua njia hiyo unakuja kufuatia tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump la kusitishwa kwa mashambulizi dhidi ya Iran ikiwa Mlango Bahari wa Hormuz utafunguliwa “kikamilifu, haraka na kwa usalama.”
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi, amethibitisha kuwa usafirishaji kupitia Mlango wa Hormuz utaendelea kwa kipindi cha wiki mbili kupitia uratibu na Vikosi vya Silaha vya Iran huku akiishukuru Pakistan kwa kuingilia kati na kuomba kusitishwa kwa vita.
Pamoja na hayo, Iran pia imesema ikiwa mazungumzo yataendelea vizuri, kipindi cha wiki mbili cha kusitisha mashambulizi kinaweza kuongezwa ambapo mazungumzo zaidi yanatarajiwa kufanyika Mjini Islamabad katika wiki zijazo ili kudumisha amani na usalama katika eneo la Ghuba ya Uajemi.
