
Wanawake wa Kitongoji cha Kirua, Kijiji cha Matala, Kata ya Mwika Kusini, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wameibua malalamiko ya kuongezeka kwa wizi wa nguo zao za ndani, wakidai huibwa wanapozianika au hata muda mfupi baada ya kutoka kuoga.
Malalamiko hayo yaliibuka Juni 1, 2026, katika mkutano wa hadhara wa kitongoji hicho uliolenga kujadili ukarabati wa barabara ili ziweze kupitika kirahisi, hasa kipindi cha mavuno.
Hata hivyo, wakati wa ajenda ya tatu iliyohusu ulinzi na usalama, wanawake wengi waligeuza mjadala na kueleza hofu yao juu ya matukio hayo ya wizi, huku hoja hiyo ikiungwa mkono na Mwenyekiti wa Kitongoji.
Mmoja wa wanawake, ambaye aliomba jina lake lisitajwe alisema tayari ameibiwa nguo zake za ndani nne katika nyakati tofauti bila kufahamu wahusika wala sababu ya kufanya hivyo.
“Nimeshaibiwa nguo zangu za ndani mara nne katika siku tofauti tofauti. Cha kushangaza zaidi, mara ya mwisho nilitoka kuoga nikaziacha kwenye beseni, lakini niliporudi sikuzikuta tena. Hadi leo sijui waliozichukua walikuwa wamejificha wapi wala walikuwa na lengo gani,” alisema.
Mwanamke mwingine alisema naye amepoteza nguo mbili za ndani katika mazingira ya kutatanisha, hali inayomlazimu kuzilinda muda wote anapozianika.
“Mwenyekiti, wewe ni mwanamke mwenzetu unaelewa hali hii. Hatuwezi kuingiza nguo za ndani zikiwa bado mbichi kwa kuhofia kupata maradhi kama UTI. Sasa tumefikia hatua ya kuzilinda tunapozianika kana kwamba tunalinda fedha au vitu vya thamani, vinginevyo kila siku utalazimika kununua nyingine,” alilalamika.
