Rais wa Laliga Amtaka Rais wa FIFA Ajiuzulu

Rais wa Laliga Amtaka Rais wa FIFA Ajiuzulu
Rais wa Laliga Amtaka Rais wa FIFA Ajiuzulu

Rais wa LaLiga, Javier Tebas, amemtaka Rais wa FIFA, Gianni Infantino, kujiuzulu kutokana na mpango unaopendekezwa wa kupanua Kombe la Dunia hadi kushirikisha mataifa 64.

Kiongozi huyo wa soka nchini Hispania alitoa kauli hiyo baada ya kumalizika kwa Kombe la Dunia la mwaka huu lililoshirikisha timu 48, mashindano ambayo yalizua mijadala na malalamiko mbalimbali.

Miongoni mwa matukio yaliyoibua utata ni pamoja na kile kilichoripotiwa kuwa Rais wa Marekani Donald Trump kuingilia kati suala la kadi nyekundu iliyopewa timu ya Marekani, mapumziko ya dakika 27 wakati wa fainali, pamoja na kusitishwa kwa mechi mara kadhaa ili wachezaji wapate maji licha ya viwanja kuwa na mfumo wa kupunguza joto.

Alipoulizwa moja kwa moja kama anaamini Infantino anapaswa kuondoka baada ya miaka 10 madarakani, Tebas hakusita kujibu.

“Kwa maoni yangu, ndiyo. Nafikiri muda wake umefika wa kuondoka,” alisema Tebas.

Hata hivyo, aliongeza kuwa Infantino bado anaungwa mkono na mfumo uliopo ndani ya FIFA pamoja na vyama vya soka duniani.

“Anaungwa mkono na mfumo na mashirikisho ya soka. Hakuna mgombea wa upinzani kwa sababu hakuna anayependa kugombea huku akijua atashindwa. Huu ni mfumo ambao una matatizo tangu kwenye msingi wake,” alisema.

Tebas aliendelea kusema kuwa:

“Sijui kama ukimya ni mbaya zaidi kuliko ushirikiano, kwa sababu wanaonyamaza wanafahamu kabisa madhara ambayo soka linaendelea kuyapata.”

Kauli zake zinakuja wakati kukiwa na hofu kwamba mpango wa kuongeza idadi ya washiriki hadi mataifa 64 katika Kombe la Dunia la mwaka 2030 unaweza kuongeza msongamano wa ratiba za soka na kuathiri ligi za ndani.

Kombe la Dunia la 2030 linatarajiwa kufanyika kwa pamoja nchini Hispania, Ureno na Morocco, huku mechi tatu za ufunguzi zikitarajiwa kuchezwa nchini Uruguay, Argentina na Paraguay kuadhimisha miaka 100 tangu kufanyika kwa Kombe la Dunia la kwanza mwaka 1930 nchini Uruguay.

Related Posts