
Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amefunguka kuwa kikosi chake kinazidi kuimarika siku hadi siku, akisifu uwezo ilionao wa kucheza na timu ‘zinazopaki basi’ kwa sasa—kitu ambacho huko nyuma ilikuwa ngumu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, kocha huyo raia wa Afrika Kusini alisema kitendo cha kutengeneza nafasi nyingi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Jumamosi iliyopita dhidi ya CFFA ya Madagascar kunaonesha ni jinsi gani walivyoimarika katika eneo hilo, ingawa sasa wanatakiwa kulifanyia kazi sehemu ya kumalizia tu. Katika mchezo huo wa mkondo wa kwanza, Yanga ilishinda mabao 4-0, huku ikiwa na kibarua rahisi cha kuzuia kufungwa mabao 5-0, kesho kwenye uwanja uliochezwa mechi ya kwanza, Azam Complex, Dar es Salaam.
“Timu hii ya Yanga inazidi kukua, lakini sina uhakika kama watu wengi wanaweza kuliona hilo. Timu hii inakua kiufundi, inaimarika katika muundo wake wa uchezaji, na inazidi kuimarika katika kutengeneza nafasi za kufunga mabao. Inazidi kuimarika katika kucheza dhidi ya timu zinazojilinda kwa wachezaji wengi nyuma. Ni vigumu sana kucheza dhidi ya timu inayokaa nyuma na kujilinda na hilo tumeliona sana kwenye Ligi Kuu tulivyokuwa tunapata ugumu, lakini kwa sasa tumepata mbinu za kuvunja safu za ulinzi za wapinzani wanaotumia mfumo huo,” alisema kocha huyo.
Alisema kwa sasa kilichobaki ni kuzitumia kwa usahihi nafasi zinazopatikana na baada ya hapo timu itakuwa tishio kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na hata kwenye Ligi Kuu ambako nyingi zinacheza kwa kuwa na wachezaji wengi nyuma ya mpira. Alisema kile kilichoonekana Jumamosi cha kuvunja ngome ya wapinzani kila walipofanya shambulizi ni matokeo ya kazi iliyofanyika kwenye uwanja wa mazoezi na si vinginevyo. “Ndiyo maana tuliweza kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, kwa sasa tunaweza kufanya hivyo kwa kila timu itakayoingia kucheza na sisi ikitaka kujilinda. Tuna tatizo moja tu la kuzitumia nafasi ambalo bado kuna kazi kubwa ya kufanya,” alisema.
Hata hivyo, wapo baadhi ya wanachama na mashabiki wamekuwa hawaridhishwi na mbinu za kocha huyo, wakidai haichezi soka la kuvutia, lakini wengine wamekwenda mbali zaidi wakidai mara nyingi mabadiliko anayoyafanya huigharimu timu badala ya kuinufaisha. Kikosi cha Yanga kitashuka dimbani kesho katika mchezo wa mkondo wa pili dhidi ya CFFA, ambapo ikipata matokeo mazuri ya jumla itatinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika
