Nature

FAMILIA ya Mdude Yapeleka Kesi Mahakama, Yakemea Utekaji

Familia ya Mdude Nyagali, mwanaharakati na mkosoaji wa serikali ambaye hajulikani alipo tangu alipotoweka kwa madai ya kutekwa na watu wasiojulikana, imechukua hatua rasmi za kisheria kwa kufungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, ikitaka haki itendeke na vitendo vya utekaji vikome.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya, mmoja wa wanafamilia hao, Christopher Faustino Nkolimwa, maarufu kama Madenge, amesema kuwa familia hiyo kwa kushirikiana na timu ya wanasheria imeamua kutumia njia halali kuhakikisha haki ya ndugu yao inapatikana kupitia mahakama.

Kesi hiyo iliyopangwa kuanza kusikilizwa rasmi tarehe 30 Juni, 2025 ilifunguliwa na Sije Emmanuel Mbugi- mke wa Mdude dhidi ya watu wengine sita ambao kati yao yumo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Mbeya.

Katika kauli yake, Madenge amedai kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kampeni ya kupinga utekaji na ukatili unaoendelea kuwakumba wananchi bila hatua madhubuti kuchukuliwa. Amesisitiza kuwa hakuna mtu aliye salama iwapo vitendo hivyo vitaachwa bila kushughulikiwa.

Mbali na hatua ya kisheria, familia hiyo imetangaza pia kuandaa kampeni ya kuchangia damu, ikiwa ni sehemu ya ujumbe wa amani na mshikamano kwa jamii. Watavaa T-shirt maalum zilizoandikwa ujumbe unaosomeka: “Changia Damu, Usimwage Damu”.

“Katika timu yetu wapo waliounganisha na Benki ya Damu. Tumeamua baada ya kutoka mahakamani, tuelekee Kituo cha Afya Kabwe tuchangie damu kwa ajili ya jamii yetu. Tunataka kutoa ujumbe wa thamani ya maisha, si vurugu na utekaji,” amesema Madenge

Related Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *