Nature

Yanga Wakana Kuichangia CCM Milioni 100, Wadai ni GSM

Klabu ya Young Africans SC (Yanga) imetoa ufafanuzi kuhusu mchango wa Shilingi milioni 100 uliotolewa katika Harambee ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) tarehe 12 Agosti 2025, kufuatia mjadala ulioibuka kwenye mitandao ya kijamii na miongoni mwa wanachama ambapo Klabu hiyo imeweka wazi kuwa fedha hizo hazikutoka kwenye akaunti wala mapato ya klabu.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya klabu hiyo iliyotolewa leo Agosti 14, 2025, fedha hizo zilitolewa na GSM Foundation taasisi inayomilikiwa na mfadhili na mdhamini wa Yanga Ghalib Said Mohammed ambapo Yanga imeeleza kuwa mchango huo ulitolewa na taasisi hiyo kwa niaba yake binafsi na si kama sehemu ya shughuli au maamuzi ya klabu.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa kwa zaidi ya miaka mitatu, GSM Foundation imekuwa mshirika wa karibu wa Yanga katika kusaidia shughuli za kijamii ndani na nje ya nchi, hivyo uhusiano huo haumaanishi kwamba kila hatua ya mfadhili wao ni ya klabu moja kwa moja. Klabu hiyo imesisitiza kuwa hakukuwa na matumizi ya fedha za wanachama wala mapato ya klabu kwenye mchango huo.

Vilevile Yanga imewaomba radhi wanachama, mashabiki na wapenzi wa mpira wa miguu nchini kwa sintofahamu yoyote iliyojitokeza kutokana na tukio hilo ikisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwaheshimu na kuwajibika kwa wafuasi wake wote.

ALSO READ | ORODHA ya Vilabu Bora Afrika 2025 (CAF Club Ranking)

Related Posts