Nature

KIMENUKA: Marekani Yaweka Zuio Kwa Watanzania Kuingia Marekani, Dhamani ya Viza Milioni 36

Serikali ya Tanzania imethibitisha kupokea rasmi taarifa kutoka Serikali ya Marekani kuhusu uamuzi wa kuiweka Tanzania katika orodha ya Nchi ambazo Raia wake watatakiwa kuweka dhamana ya viza (visa bond) kabla ya kuingia Nchini humo kwa madhumuni ya biashara (viza za B-1) au madhumuni ya utalii (viza za B-2) ambapo masharti hayo mapya yanatarajiwa kuanza kutumika rasmi kuanzia 23 Oktoba 2025.

Hii inamaanisha kuanzia October 23, 2025 Watanzania na Raia wa Mataifa mengine kadhaa wanaoomba visa za B-1 (biashara) na B-2 (Utalii) watatakiwa kuweka dhamana (bond) ya kuanzia USD 5000 (Tsh. milioni 12+) hadi USD 15000(Tsh. milioni 36+) ili wapewe fursa kuingia Marekani na hivyo kuifanya Tanzania kuingia kwenye orodha ya Nchi za Afrika zilizowekea sharti hilo zikiwemo Malawi, Zambia, Gambia, Mali na Mauritania.

Uamuzi huo umefikiwa kufuatia utafiti uliofanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani Marekani mwaka 2024 ambao ulizitaja Nchi kadhaa kuwa na idadi kubwa ya Watu ambao wakiingia Marekani wanapitiliza muda wa kukaa na wengine hufikia hatua ya kuzamia na kubakia Marekani licha ya visa zao kuisha ambapo kwa masharti haya mapya wale watakaorudi nchini mwao ndani ya muda sahihi watarudishiwa fedha zao wakirudi kwenye nchi zao lakini wale watakaozidisha muda wa kukaa Marekani au kukiuka kanuni zozote za visa pesa zao walizoweka dhamana hazitorudishwa.

Watu ambao watapewa visa chini ya masharti haya mapya watatakiwa kuingia Marekani na kuondoka kupitia Airport maalum ikiwemo Boston Logan International Airport(BOS), John F Kennedy Internation Airport (JFK) na Washington Dulles International (IAS) lengo likiwa ni kuweka urahisi wa ufuatiliaji wa utekelezwaji wa masharti mapya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa, hatua hiyo ya Marekani imekuja wakati ambapo majadiliano kuhusu masuala ya uhamiaji baina ya Marekani na Tanzania yakiendelea ambapo Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa itaendeleza majadiliano hayo kwa njia za kidiplomasia ili kutafuta suluhisho la haki linalozingatia usawa na maslahi ya pande zote.

Related Posts