Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP) Sylvester Mwakitalu amewafutia kesi na kuwaachia huru Washtakiwa 210 waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama na kutenda kosa la uhaini ambapo Washtakiwa hao wameachiwa leo Novemba 24, 2025 katika Mahakama za Mkoa wa Dar es salaam, Arusha na Mwanza.
Itakumbukwa kuwa siku kumi zilizopita (Novemba 14,2025) akizindua Bunge la 13 Jijini Dodoma Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alimuagiza Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwasamehe Vijana waliofanya makosa kwa kufuata mkumbo.
Jumla ya Watuhumiwa 139 waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya uhaini Jijini Mwanza ikiwemo kuchoma moto, kuharibu mali za umma na unyang’anyi wa kutumia silaha kutokana na vurugu za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 wameachiwa huru baada ya DPP kuondoa kesi zao Mahakamani katika Mahakama za Wilaya za Ilemela na Nyamagana.
Uamuzi huo umekuja baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha maombi ya DPP ya kuonesha nia ya kutotaka kuendelea na mashtaka dhidi yao ambapo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam DPP amewafutia kesi na kuwaachia huru Washtakiwa 47 waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama za kutenda na kosa la uhaini.
Kwa Mkoa wa Arusha Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha leo Novemba 24 pia imewaachia huru na kuwafutia mashtaka ya uhaini Washtakiwa 24 waliokuwa wakishtakiwa kwa makosa mawili ya kula njama na kutenda uhaini ambapo uamuzi huo umefikiwa leo na Hakimu Mkazi Mfawidhi Erasto Philly baada ya Mawakili wa Serikali kuieleza Mahakama kuwa DPP hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya Washtakiwa hao.
Washtakiwa hao wamefutiwa kesi hiyo chini ya kifungu namba 92(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023.

