Afariki baada ya kipigo cha mpenzi wake, mtuhumiwa ajinyonga

Afariki baada ya kipigo cha mpenzi wake, mtuhumiwa ajinyonga
Afariki baada ya kipigo cha mpenzi wake, mtuhumiwa ajinyonga

Mwanamke mwenye umri wa miaka 47, Helena Matiku, mhudumu wa baa na mkazi wa Musoma, amefariki dunia baada ya kudaiwa kupigwa kwa ngumi na mateke na mpenzi wake, ambaye baadaye alijinyonga hadi kufa.

Tukio hilo limetokea Agosti 5, 2026 katika nyumba ya kulala wageni ya Siti, iliyopo Kisiwa cha Kunene, Kijiji cha Busumba, Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa, amesema mtuhumiwa huyo ametambuliwa kwa jina la Fabian Makamba (33), mvuvi na mkazi wa Kigeretuma, Wilaya ya Musoma Vijijini, ambaye alikuwa mpenzi wa marehemu.

Kwa mujibu wa Kamanda Mtafungwa, ugomvi ulianza baada ya Helena kuuza nguo za mpenzi wake akidaiwa kufanya hivyo kutokana na kunyimwa fedha za matumizi. Hali hiyo ilimkasirisha Fabian ambaye alidaiwa kumpiga kwa ngumi na mateke sehemu mbalimbali za mwili.

Baada ya kushambuliwa, Helena hakutoa taarifa polisi wala kwenda hospitalini kwa ajili ya matibabu. Hata hivyo, Agosti 10, afya yake ilipozidi kuwa mbaya, alikwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure kwa ajili ya matibabu.

“Wakati akiendelea kupatiwa matibabu, Agosti 11, mwaka huu, majira ya saa 5:00 usiku, alifariki dunia,” amesema Kamanda Mtafungwa.

Kamanda huyo amesema Jeshi la Polisi lilipoanza kufuatilia tukio hilo, Fabian alikutwa Agosti 11, majira ya saa 2:30 asubuhi, akiwa amejinyonga hadi kufa.

Amesema mtuhumiwa alidaiwa kuchukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa mpenzi wake amefariki dunia kutokana na kipigo, akihofiwa kuwa alifanya hivyo kwa lengo la kukwepa mkono wa sheria.

Kamanda Mtafungwa amesema chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa kifamilia na amewataka wananchi kuepuka kutumia nguvu au kujichukulia sheria mkononi wanapokabiliwa na migogoro ya kifamilia.

Aidha, amewahimiza wananchi kutumia vyombo vya sheria, viongozi wa dini na maafisa ustawi wa jamii katika kutatua migogoro, badala ya kutumia vitendo vya ukatili.

Pia amewataka wananchi kutoa taarifa mapema katika vituo vya polisi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili na kwenda hospitalini mara moja wanapopata madhara, ili kupata matibabu na msaada wa kisheria kwa wakati.

Related Posts