
Marekani imetangaza kuanza kufanya tathmini ya kina ya uhusiano wake wa kibalozi na Serikali ya Tanzania, ikieleza kuwa hatua za hivi karibuni za Serikali ya Tanzania zimezua wasiwasi mkubwa kuhusu usalama, demokrasia na mazingira ya uwekezaji nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Naibu Msemaji Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Tommy Pigott, kupitia tovuti ya Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, Washington imeeleza kile ilichokitanabaisha kuwa matukio mbalimbali ya kukandamiza uhuru wa dini na uhuru wa kujieleza, pamoja na kuwepo kwa vikwazo kwa wawekezaji wa Marekani, yameifanya ianze kupitia upya mustakabali wa ushirikiano wake na Tanzania.
“Marekani inathamini ushirikiano wake wa muda mrefu na watu wa Tanzania, ambao umeleta ustawi kwa wananchi wetu na usalama katika kanda hii. Hata hivyo, hatua za hivi karibuni za Serikali ya Tanzania zimezua wasiwasi mkubwa kuhusu mwelekeo wa uhusiano wetu rasmi wa kibalozi na kuaminika kwa Serikali ya Tanzania kama mbia”, imeeleza taarifa hiyo.
Pigott amesema vitendo vinavyoendelea kuripotiwa nchini, ikiwemo “ukatili dhidi ya raia kabla na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29,” vimeongeza wasiwasi kuhusu kuaminika kwa Serikali ya Tanzania kama mbia wa muda mrefu wa Marekani.
Aidha, Marekani imeeleza kuwa hatua hizo zimeweka hatarini raia wake, watalii na maslahi yake ndani ya Tanzania, jambo ambalo linaweza kudhoofisha ustawi na usalama wa pamoja uliojengwa kwa miongo kadhaa kati ya mataifa hayo mawili.
“Marekani haiwezi kufumbia macho vitendo vinavyohatarisha usalama wa raia wetu, au utulivu wa kanda,” imesema taarifa hiyo, ikiongeza kuwa mustakabali wa uhusiano wa kibalozi utategemea hatua zitakazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kipindi kijacho.

