Nature

Simbachawene Awapa Polisi Maagizo Mapya ya Kukamata Watuhumiwa Kiholela

George Simbachawene Waziri wa mambo ya ndani ya Nchi, ameagiza jeshi la polisi kuhakikisha kuwa taratibu za ukamataji watuhumiwa zinafanyika kwa kufuata sheria,weledi na staha.

Akizungumza leo tarehe 8 Decemba 2025 wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari, Simbachawene amesema aina ya ukamataji unaofanywa na baadhi ya askari ikiwemo kuvaa kininja, kutovaa sare rasmi za polisi na kwenda kuwakamata watuhumiwa majumbani usiku haukubaliki na unapaswa kusitishwa.

“Ukamataji ninaoutaka mimi ni ule wa kisheria, askari anaenda, anaripoti kwa mjumbe, mtu anajulikana yupo kazini kwake, kwanini uende kumkamata nyumbani kwake umevaa kininja? Tumekubaliana kwamba kuwe na ukamataji wenye staha,” amesema.

Ameongeza kuwa Jeshi la polisi linapaswa kuzingatia uwiano kati ya ukubwa wa kosa na namna hatua za kisheria zinavyotekelezwa ili kuepusha matukio yanayoweza kuwatia hofu wananchi.

“Masuala ya kiusalama ni mengi, mambo kama haya lazima yaendane na tukio lenyewe. Si kosa dogo tu, mtu kaposti kitu mtandaoni halafu anakamatwa usiku na askari wenye silaha nzito. tumekubaliana haya hayawezi kuendelea,” amesema na kuongeza kuwa baadhi ya mbinu hizo zimekuwa zikichochea chuki za wananchi dhidi ya polisi na kuathiri taswira ya jeshi hilo

Related Posts