Mwanariadha Simbu Aipa Heshima Tena Tanzania Huko India

Mwanariadha wa Tanzania na Jeshi la Wananchi (JWTZ), Alphonce Felix Simbu, ameendelea kuonyesha kiwango cha juu kimataifa baada ya kumaliza nafasi ya pili katika mbio za Kolkata 25KM zilizofanyika leo Jumapili, Desemba 21, 2025 Kolkata India.

Katika mbio hizo, Simbu alitumia saa 1:11:56 kumaliza wa pili nyuma ya Joshua Cheptegei wa Uganda aliyeshinda kwa saa 1:11:49, huku ushindani ukiwa mkali kati ya wanariadha hao bora.

Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Tebello Ramagoana wa Lithuania alietumia saa 1:11:59, wakati Collins Kipkorir wa Kenya alimaliza nafasi ya nne kwa saa 1:12:02.

Kwa upande wa Wanawake, wanariadha wa Ethiopia walitawala kwa kuchukua nafasi nne za juu, Degitu Azimeraw akiibuka mshindi kwa saa 1:19:36 , akifuatiwa na Situme Kabede kwa saa 1:20:28, Meselech Alemayehu kwa saa 1:20:48 na Kuftu Tayri kwa saa 1:23:32.

Matokeo hayo yanaendeleza mafanikio ya Simbu mwaka huu, ikiwemo kumaliza nafasi ya pili katika Boston Marathon, Marekani, kushinda medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia yaliyofanyika Septemba Tokyo, Japan, na kuweka rekodi ya Mtanzania wa kwanza kushinda marathoni za dunia.

Pia aliingia kwenye fainali ya mwanariadha bora wa kiume wa mwaka 2025, kipengele cha wanariadha wanaokimbia nje ya uwanja, napo aliweka rekodi ya kuwa Manzanita wa kwanza kuingia fainali za tuzo zinazoandaliwa na Shirikisho la riadha la dunia.

Shirikisho la riadha la Tanzania (RT), limeeleza kuwa mafanikio ya Simbu yanaendelea kuitangaza Tanzania kimataifa na kuchochea maendeleo ya riadha nchini, huku yakitajwa kuwa chachu kwa wanariadha chipukizi kuamini uwezo wao kujituma zaidi.

Rais wa RT, Rogath John amempongeza Simbu kwa kushika nafasi hiyo na kuongeza kuwa kama viongozi wanafurahi kuona mafanikio ya wale ambao wanawasimamia.

“Simbu ni mpambanaji sana, pongezi kwake na taasisi yake ya Jeshi la Wananchi (JWTZ), pia kocha wake Antony Mwingereza ambao wamekuwa nae bega kwa bega kuhakikisha mafanikio mengi zaidi yanapatikana”.

Related Posts