
Dereva Aliyetishia Kwa Bastola Bandia Dodoma Akamatwa
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linamshikilia dereva wa TARURA, Wilaya ya Dodoma, Sath John Masawa (31) kwa kosa la kumtisha kwa kitu kilichodhaniwa kuwa ni bastola dereva wa basi la SATCO lenye usajili namba T308 EME aina ya Yutong aitwaye Said Fadhili (54) wakati akiwa anatoka kuweka mafuta katika kituo cha Total Energies.
Taarifa ya leo Septemba 22, 2026 iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Gallus Hyera imeeleza kuwa tukio hilo linadaiwa kutokea baada ya Said Fadhili kudaiwa kukwangua gari mali ya TARURA lenye usajili namba STM 5806, aina ya Land Cruiser LX 70 Series, lililokuwa likiendeshwa na Mtuhumiwa huyo.
Baada ya tukio hilo kuripotiwa, Jeshi la Polisi lilifika eneo la tukio na kumkamata Sath John na baada ya kufanya upekuzi lilifanikiwa kutambua kuwa kitu alichokuwa amevaa kiunoni ni bastola bandia (toy) na siyo silaha halisi kama ilvyodhaniwa na wananchi.
Jeshi la Polisi liligundua kuwa gari hilo lilikuwa halitumii namba za usajii halisi ambazo ni STM 5806 mali ya TARURA wakati wa tukio hilo bali namba za usajli T 881 ENZ ambayo ni gari mali ya mtu mwingine na linamshikilia mtuhumiwa kwa ajii ya mahojiano na hatua zaidi za kisheria.
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limetoa onyo kwa madereva kuacha kutumia namba bandia za magari na kwa kufanya hivyo kunaficha utambulisho halisi wa gari kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa sheria.
