
Aliyeingia CRDB na kudai apewe fedha ya kula, auawa kwa risasi
Mwanamume anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30 na 35, ambaye bado hajafahamika jina wala makazi yake, amefariki dunia baada ya kupigwa risasi na polisi kufuatia tukio la kuvamia Benki ya CRDB, Tawi la Rock City Mall, Wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari leo Kamanda ya polisi mkoa wa Mwanza Wilbord Mutafungwa anaeleza kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 13, 2026 majira ya saa 7:58 mchana, baada ya mwanamume huyo kuingia ndani ya benki hiyo akiwa kama mteja na kuwalazimisha wahudumu kumpatia fedha.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, mwanamume huyo alikuwa amevaa kofia aina ya kapero, shati la mikono mirefu, suruali nyeusi ya jeans na viatu vya wazi.
Inaelezwa kuwa baada ya kufika katika sehemu ya kutolea huduma kwa wateja, alimuomba mhudumu ampatie fedha akidai ni kwa ajili ya kula.
Mhudumu huyo alimwelekeza utaratibu wa kutoa na kuweka fedha, lakini mwanamume huyo aliendelea kusisitiza apewe fedha za kula.
Kutokana na hali hiyo, mhudumu alihisi kuwa kuna hatari na kuamua kwenda kwa wafanyakazi wenzake ili kupata msaada
hata hivyo, mwanamume huyo aliruka kaunta ya sehemu ya huduma kwa wateja na kuelekea moja kwa moja katika vyumba vya kuhesabia fedha, ambapo alimsukuma mhudumu na kuingia naye ndani ya chumba hicho.
Kitendo hicho kilizua hofu na taharuki miongoni mwa wafanyakazi na wateja waliokuwa wakipata huduma katika benki hiyo.
Anaeleza kuwa polisi waliokuwa wakitoa ulinzi katika benki hiyo walifika eneo la tukio na kumtaka mwanamume huyo kujisalimisha, lakini inadaiwa alikaidi amri hiyo na kuanza kupambana na askari, huku akijaribu kuwasogelea na kutaka kuwanyang’anya silaha.
Kwa mujibu wa Mtafungwa anaeleza kuwa , licha ya kutakiwa kujisalimisha na kukaa chini, mwanamume huyo aliendelea kukaidi, hali iliyowafanya askari kuamua kumdhibiti kwa kumpiga risasi.
“Risasi hiyo ilimpiga sehemu ya kiunoni upande wa mguu wa kulia na kumsababishia jeraha lililosababisha kuvuja damu nyingi alikimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu, lakini alibainika kuwa amefariki dunia chanzo cha tukio hilo ni tamaa ya fedha.”anaeleza
Aidha anaeleza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou-Toure kwa ajili ya utambuzi na hatua nyingine za uchunguzi.
Pia katika upekuzi uliofanyika baada ya tukio, marehemu alikutwa na simu moja aina ya Samsung yenye rangi nyeusi pamoja na Sh500.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo, huku likitoa onyo dhidi ya vitendo vya uhalifu na kusisitiza kuwa litachukua hatua za kisheria dhidi ya watakaokiuka sheria.
