Chama Amvaa HansRafael Kwa Kudai Ameshuka Kiwango

Chama Amvaa HansRafael Kwa Kudai Ameshuka Kiwango

Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Simba SC, Clatous Chama, amemjibu mchambuzi wa michezo wa kituo cha redio cha Crown FM, Hans Rafael, kufuatia kauli zake za hivi karibuni zinazodai kuwa nyota huyo ameshuka kiwango na hajitumi ipasavyo uwanjani.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Hans Rafael aliibua mjadala mzito miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka nchini baada ya kulinganisha kiwango cha kiungo huyo raia wa Zambia kabla na baada ya kusaini mkataba mpya klabuni hapo.

Katika andiko lake, mchambuzi huyo aliandika kuwa kuna Chama anayesaka mkataba mpya halafu kuna Chama mwenye mkataba mpya, akisisitiza kuwa wawili hao wakikutana watapigana hadi kesho kutokana na tofauti kubwa ya ari na uchezaji wao.

Rafael aliendelea kufafanua kuwa yule Chama wa msimu uliopita ambaye alikuwa akitafuta mkataba mpya ndani ya Simba SC alikuwa wa moto sana uwanjani, tofauti na huyu wa msimu huu ambaye alidai anazidi kushuka kiwango kila kukicha.

Hata hivyo, Chama hakukaa kimya ambapo alimjibu mchambuzi huyo kwa lugha ya kistaarabu kupitia mitandao ya kijamii, akionyesha kutokubaliana na mtazamo huo huku akijivunia mwenendo mzuri na mafanikio ya timu yake ya Simba SC kwa sasa.

Katika majibu yake, nyota huyo alieleza kuwa pamoja na ukosoaji huo bado timu inaendelea kupata ushindi uwanjani, akimpongeza mchambuzi huyo kwa kazi yake na kumtabiria kufika mbali zaidi katika vituo vikubwa vya kimataifa kama BBC au CNN.


Chama alihitimisha majibu yake kwa ujumbe wa kifalsafa akisema kuwa maisha yana usawa wa hali ya juu, kwani siku zake mbaya kwake ndizo siku njema kwa mchambuzi huyo, hivyo alimtakia heri na kumtaka aendelee kufurahia nyakati zake.

Related Posts