
Dar es Salaam . Tishio la mlipuko na kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola katika nchi za DR Congo na Uganda, limesababisha mechi mbili za kimataifa za kirafiki ambazo timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ilipanga kuzicheza dhidi ya Uganda na Rwanda Ijumaa hii na Jumanne wiki ijayo jijini Marrakech, Morocco kufutwa.
Uamuzi wa kufutwa mechi hizo na nyinginezo zilizopangwa kuchezwa nchini humo, umetolewa na serikali ya Morocco kama miongoni mwa hatua za kujikinga na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ambao umeonekana kusambaa na kuanza kuleta athari hasi kwa nchi za DR Congo na Uganda
Mchezo wa kwanza ulikuwa uwe dhidi ya Uganda, Juni 5 na wa pili ulipangwa kuchezwa Juni 9 dhidi ya Rwanda.
Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Oscar Mirambo amethibitisha juu ya hilo.
“Ni kweli hizo mechi zimefutwa na tutatoa taarifa rasmi muda mfupi ujao,” amesema Mirambo.
Kabla ya taarifa ya mechi za Taifa Stars, Shirikisho la Mpira wa Miguu Madagascar, lilitoa taarifa ya mechi za timu yake ya taifa ambazo zilipangwa kucheza Morocco zimefutwa.
“Tumepokea taarifa kutoka kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Morocco la kufutwa kwa mechi zote za FIFA Series 2026.
“Uamuzi huu unatokana na miongozo ya mamlaka za Morocco ambazo zimeelekeza kwamba hakuna kusanyiko lolote linalopaswa kufanyika katika kipindi hiki cha Juni kutokana na tahadhari za kiafya,” imefafanua taarifa ya Shirikisho la Soka Madagascar.
