Form 6 Waliotaka Kuchoma Milambo SEC Wakamatwa

Wahitimu wa kidato cha sita zaidi ya 130 katika Shule ya Sekondari Milambo iliyopo Mkoani Tabora wamelazimika kuondolewa Shuleni hapo chini ya ulinzi mkali wa Jeshi Polisi muda mfupi baada ya kumaliza mtihani wao wa mwisho wa kuhitimu kidato cha sita, hii ikiwa ni baada ya njama zao za kutaka kuchoma Shule hiyo na kuandamana kubainika.

Wanafunzi hao wanatuhumiwa kupanga njama hizo baada ya kuzuiwa kufanya mahafali ya kuhitimu masomo yao kutokana na kile ambacho Shule imesema ni uwepo wa viashiria vya uvunjifu wa amani kwakuwa Uongozi wa Shule ulipata taarifa kuwa Wanafunzi walipanga kufanya vurugu kali Shuleni baada tu ya mahafali kumalizika.

Uongozi wa Shule umesema sababu nyingine iliyofanya wasiruhusu mahafali kufanyika ni kwakuwa Wanafunzi hao baada ya kuona wanakaribia kuhitimu Shule walianza tabia za hovyo ikiwemo kufanya jogging mitaani wakiwa na muziki mkubwa huku wakiwa wamevua nguo, kujichora tattoo, kutoroka na kwenda club usiku na wakirudi wanazima umeme wa Shule nzima ndipo wanaingia mabwenini pamoja na kuanzisha mabifu na ugomvi na Shule jirani na hata kupigana nao wakati wa mechi au michezo ya jioni.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Paul Chacha, ameelekeza Wanafunzi hao waondolewe Shuleni hapo na kwenda makwao chini ya ulinzi huku akiwataka Polisi kuimarisha ulinzi maeneo yote ya Shule kwani baadhi ya Wanafunzi wa madarasa mengine wengine wanaendelea na masomo na pia kundi jingine la kidato cha sita linaendelea na mitihani chini ya ulinzi mkali wa Polisi na wakishamaliza tu nao watapelekwa makwao .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *