Gari Lililoibiwa Lakutwa Kwa Fundi Magari Songwe

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limefanikiwa kulikamata gari lililoibiwa aina ya Mitsubishi Outlander pamoja na mtuhumiwa mmoja, ambaye alikutwa akiwa na bastola ya kutengeneza kienyeji, kufuatia msako mkali uliofanywa na Jeshi hilo.

Tukio hilo linahusiana na wizi wa gari uliotokea tarehe 16 Desemba, 2025 saa 06:00 usiku katika Mtaa wa Uwanjani, Tarafa ya Tunduma, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe. Gari hilo aina ya Mitsubishi Outlander lenye namba za usajili T.897 EAC, chasis namba CW5W0008014 na engine namba 4B12AA5184, lenye thamani ya Shilingi 20,000,000/=, ni mali ya Jovin Kafana (37), mfanyabiashara (Agent), mkazi wa Tazara, Mji wa Tunduma, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe.

Gari hilo liliibiwa baada ya mmiliki wake kuvamiwa na majambazi waliomtishia kwa kutumia bastola ya kutengeneza kienyeji. Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianza mara moja jitihada za kuwatafuta watuhumiwa hao.
Baada ya kuendelea na msako mkali, tarehe 06 Februari, 2026 saa 17:30 jioni, askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe walipata taarifa za kiintelijensia kuwa gari hilo lilikuwa eneo la Makambako, Mkoa wa Njombe. Askari walifika Makambako na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa aitwaye Bashiru Madembwe (35), fundi magari na mkazi wa Makambako, Mkoa wa Njombe. Mtuhumiwa huyo aliwaonesha askari mahali alipolificha gari hilo katika Kitongoji cha Ipilimo, Kijiji cha Iyai, Kata ya Ihowanza, Tarafa ya Malangali, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja (jina limehifadhiwa kwa ajili ya upelelezi) aliyehusika katika tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha lililotokea tarehe 04 Februari, 2026 saa 04:00 asubuhi, katika eneo la Kisimani, Mtaa wa Unyamwanga, Kata ya Tunduma, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe.
Katika tukio hilo, mtuhumiwa huyo akiwa na wenzake walimfyatulia risasi Yengo Mwapina, mkazi wa Sogea, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe, na kumsababishia jeraha katika kiuno upande wa kushoto, pamoja na kumnyang’anya fedha kiasi cha Shilingi 54,000,000/= akiwa anatoka katika Benki ya NBC Tunduma.

Watuhumiwa hao wanaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano ili kubaini mtandao wao na watu wengine wanaoshirikiana nao katika vitendo vya ujambazi na unyang’anyi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Baada ya kukamilika kwa mahojiano, hatua za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi yao kwa mujibu wa sheria.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linatoa onyo kali kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo vya ujambazi, unyang’anyi wa kutumia silaha na uhalifu wa aina yoyote kuwa hakuna mahali pa kujificha, kwani Jeshi lina mtandao mpana wa kiintelijensia na linaendelea kufanya operesheni kali, endelevu na zisizotabirika. Aidha, Jeshi linawakumbusha wahalifu kuwa mkono wa sheria ni mrefu na yeyote atakayejihusisha na vitendo hivyo atakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Vilevile, Jeshi la Polisi linaendelea kuwaomba wananchi kushirikiana nalo kwa kutoa taarifa za wahalifu na vitendo vya kihalifu, kwani usalama ni jukumu la kila mmoja wetu.

Related Posts