Kenya Hatarini Kupoteza Haki ya Kuandaa Afcon 2027 Kwa Kushindwa Kulipa Ada


Afisa Mkuu wa Serikali ameonya kuwa Kenya iko katika hatari kubwa ya kupokonywa haki ya kuandaa michuano ya Africa Cup of Nations (AFCON) 2027 kutokana na changamoto za kifedha pamoja na ucheleweshaji wa ujenzi na ukarabati wa viwanja.

Katibu Mkuu wa Michezo, Elijah Mwangi, alifichua mbele ya Wabunge kwamba nchi bado haijalipa ada ya lazima ya Ksh 3.9 bilioni (takribani dola milioni 30) inayotakiwa kulipwa kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mgogoro wa fedha unaendelea kuathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya ukarabati wa viwanja muhimu vitakavyotumika kwenye mashindano hayo.

Mwangi alibainisha kuwa viwanja vya Kasarani na Nyayo huenda vikawa tayari ndani ya muda wa miezi sita uliowekwa na CAF, ingawa kuna changamoto za kifedha zinazoendelea kuchelewesha kazi.

Aidha, alieleza kuwa mkandarasi anayekarabati Uwanja wa Kasarani amepunguza idadi ya wafanyakazi kutokana na deni la Serikali linalofikia zaidi ya Ksh 3.7 bilioni. Hali katika Uwanja wa Nyayo nayo imeelezwa kuwa mbaya zaidi, ambapo mkandarasi amesitisha sehemu kubwa ya kazi kutokana na malimbikizo ya malipo yanayozidi Ksh 2.6 bilioni.

Related Posts