Kibano ufungaji holela ving’ora na Vimuli muli Kwenye Magari

Kibano ufungaji holela ving’ora na Vimuli muli Kwenye Magari
Kibano ufungaji holela ving’ora na Vimuli muli Kwenye Magari

Kibano ufungaji holela ving’ora na Vimuli muli Kwenye Magari

Baada ya kilio cha muda mrefu cha watumiaji wa barabara nchini, hatimaye Serikali imeweka sheria ya kudhibiti ufungaji holela wa ving’ora na vimulimuli kwenye magari yasiyo na kibali, huku ikiweka faini ya hadi Sh300,000.
Sheria hiyo, ambayo imepongezwa na wadau, wakiwamo mawakili, imetaja makundi saba ya viongozi wa Serikali ambao misafara yao itaruhusiwa kuwa na vifaa hivyo pamoja na rangi maalumu za vimulimuli. Miongoni mwao ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar.

Kanuni hizo zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, zimeonya kuwa mtu atakayefunga vifaa hivyo nje ya makundi hayo saba bila kibali cha waziri, atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia anaweza kutozwa faini ya hadi Sh300,000.

Kwa muda mrefu imekuwa kawaida kwa baadhi ya madereva wanaoendesha magari ya kifahari, yakiwamo Toyota Land Cruiser na mengine yanayofanana nayo, kufunga vifaa hivyo kiholela ili waonekane kama ‘vibosile’ wasiostahili kusimamishwa na askari wa usalama barabarani.

Magari mengine ni ya watu binafsi wasio na uhusiano na Serikali, ambao hawako kwenye misafara wala hawana kibali cha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, lakini wamekuwa wakifunga vifaa hivyo kiholela na kujifanya magari ya ‘vibosile.’

Mbali na magari hayo, hivi sasa imekuwa jambo la kawaida kukuta mabasi makubwa yakiwa yamefungwa vimulimuli na ving’ora, huku baadhi ya pikipiki nazo zikifungwa taa zinazowaka na kuzima (flashing beacon) pamoja na ving’ora.

Baadhi ya magari hayo yamekuwa yakitumika kama kichaka cha kuficha uhalifu, ikiwamo kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi, kwa kuwa ni nadra magari yenye kimulimuli kinachoonekana kwenye kioo cha mbele cha dereva kusimamishwa na kukaguliwa.

Hali hiyo inatajwa kuchangiwa na baadhi ya askari wa usalama barabarani au polisi katika vituo vya ukaguzi kujenga hisia kuwa magari yenye vifaa hivyo ni ya ‘wakubwa’, hivyo kuhofia kuyasimamisha na kuwahoji madereva wake, kumbe pembeni yake kunaweza kuwa na mtu mwenye nafasi kubwa katika chombo nyeti.

Wadau wa usafirishaji waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wamepongeza hatua hiyo, wakisema sheria hiyo imegusa magari ambayo yamekuwa kero barabarani, ambako ni vigumu kutofautisha kama linalopita ni sehemu ya msafara rasmi au ni la mtu binafsi.

Kanuni hizo za mwaka 2026, zinazotokana na Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, zimetangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) Juni 19, 2026, lakini zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii ya wadau wa usafiri Agosti 13, 2026.

Kwa mujibu wa tafsiri ya kanuni hizo, zinaitwa Kanuni za Usafiri wa Barabarani (Siren, Ishara za Sauti, Filimbi na Taa za Tahadhari zinazowaka na Kuzima), 2026.

Kanuni hizo zinafafanua sireni kuwa ni kifaa kinachotoa sauti kubwa (king’ora) na ya muda mrefu ya onyo.

Wakili wa Mahakama Kuu, Peter Kibatala amesema kila mtu ana wajibu wa kuheshimu sheria za nchi kwa mujibu wa Ibara ya 26(1) ya Katiba.

“Hiyo kanuni ni sheria kama sheria nyingine. Imeweka makundi ya nani wanastahili kufunga ving’ora na vimulimuli. Kama hujatajwa na sheria basi unatenda kosa la jinai. Maana kila mmoja akijifungia tu ni fujo,” amesema.

Naye, Wakili Peter Mshikilwa amesema changamoto kubwa itakuwa katika usimamizi wa sheria, akitaka pia kuwepo kwa udhibiti wa uagizaji na uuzaji wa vifaa hivyo.

“Kwa sababu haingii akilini anayeagiza anauza kwa walaji bila kuulizwa au kutoa taarifa anamuuzia mtu yupi na ambaye ana haki ya matumizi. Kwa ufupi kuna shida kwenye usimamizi wa sheria na kanuni zetu,” amesema.

Wakili mwingine wa Mahakama Kuu, Dk Rwezaura Kaijage amesema matumizi ya ving’ora na vimulimuli yalianza kama mzaha, lakini yameenea hadi kwenye bajaji na bodaboda.

Amesema GN namba 151 ya 2026 imekuja wakati muafaka, lakini utekelezaji wake unapaswa kufanyika bila ubaguzi.

Kanuni hizo zimetungwa chini ya Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, na kutangazwa katika Gazeti la Serikali Juni 19, 2026.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, zinaitwa Kanuni za Usafiri wa Barabarani (Siren, Ishara za Sauti, Filimbi na Taa za Tahadhari zinazowaka na Kuzima), 2026, na zimefafanua sireni kuwa ni kifaa kinachotoa sauti kubwa na ya muda mrefu ya onyo.

RSA, wananchi wanena haya
Mwenyekiti wa Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA) Mkoa wa Kilimanjaro, Khalid Shekoloa ameipongeza Serikali kwa kuweka kanuni za kudhibiti matumizi ya vimulimuli na ving’ora, akisema si sahihi kila mmiliki wa gari kufunga vifaa hivyo bila kuwa na dhamana maalumu.

“Kanuni hizi zinakwenda kuwadhibiti wale ambao hawakuwa na dhamana ya kutumia vifaa hivi. Kwa sasa itakuwa rahisi kwa vyombo vya usalama kuwachukulia hatua. Napongeza sana ujio wake,” amesema Shekoloa.

Mfanyabiashara wa Dar es Salaam, Amani Ngowi amesema baadhi ya wamiliki wa magari yenye namba za usajili zinazoanzia herufi E, hasa Toyota Land Cruiser, wamekuwa wakiamini kuwa wana haki ya kufunga vimulimuli na ving’ora.

“Si viongozi tu, hata baadhi ya matajiri wanaona ni haki yao. Tatizo la nchi hii ni kwamba hata sheria zinapotangazwa, hazifuatwi,” amesema.

Amesema matumizi ya vimulimuli yameenea hadi kwenye bajaji, mabasi na malori, hali inayofanya wakati wa usiku kuwa vigumu kutambua kama gari linalokuja ni la wagonjwa, la kiongozi au la mtu binafsi.

“Nakumbuka zamani kulikuwa na RTO (Mkuu wa Usalama Barabarani) wa Iringa aliyesimamia sheria hiyo. Akikukamata, aliondoa vifaa hivyo. Vimilimuli kwenye vioo vya mbele ni usumbufu mtupu,” amesema.

Kwa upande wake, mjasiriamali wa Arusha na Kilimanjaro, Renalda Mbore, amesema uamuzi huo ni mzuri iwapo utatekelezwa ipasavyo, akiwataka askari wa usalama barabarani kutekeleza sheria bila woga.

Mbore pia amependekeza kiwango cha faini kwa wanaokiuka sheria hiyo kiongezwe hadi Sh500,000 ili kiwe na nguvu zaidi katika kuzuia matumizi holela ya vifaa hivyo.

Dereva wa teksi mjini Moshi, Baraka Matemba, amesema sheria hiyo ni nzuri, lakini changamoto imekuwa katika utekelezaji wake, akidai baadhi ya wanaopewa dhamana ya kusimamia sheria wamekuwa wakishindwa kuwachukulia hatua wahusika.

“Sasa hivi wananchi wameanza kudharau ving’ora, maana hata baadhi ya bodaboda wamevifunga. Kumekuwa hakuna heshima tena hata kwa ambulensi kwa sababu kila mtu amefunga chake. Kuviwekea sheria ngumu ni sawa,” amesema.

Matemba amesema udhibiti huo utasaidia kurejesha heshima ya vifaa hivyo, kwani mtumiaji wa barabara akisikia king’ora ataelewa kuwa kuna gari lenye dharura, hivyo kutoa nafasi.

Ameongeza kuwa iwapo kuna uwezekano wa kuongeza faini, hatua hiyo ifanyike ili kuwazuia watu wasio na dhamana kufunga na kutumia ving’ora na vimulimuli.

Kanuni zinasemaje?
Kanuni ambazo zimechapwa katika Gazeti la Serikali namba 151, zimeweka madhumuni makuu matatu huku moja ikieleza ni nani anaruhusiwa kutumia sireni, ishara za sauti, filimbi na taa zinazong’ara kwenye magari barabarani.

Ya pili, inataja ni nani wanaruhusiwa kutumia taa hizo kwa maana ya vimulimuli na ving’ora; inataja kuwa ni magari ya viongozi wa ngazi za juu na magari ya dharura yaliyoidhinishwa kama Zimamoto, Ambulensi na Polisi.

Tatu, kanuni inataja rangi za taa na sireni; ni matumizi kwa viongozi; kwa misafara ya Rais, zitakuwa ni taa nyekundu-nyeupe-nyekundu na king’ora, kwa makamu wa Rais na Rais wa Zanzibar nyekundu-nyeupe-bluu na king’ora.

Kwa upande wa waziri mkuu, naibu waziri mkuu au makamu wa pili wa Rais Zanzibar zitakuwa taa za chanja-nyeupe-bluu na king’ora wakati spika wa Bunge, jaji mkuu wa Tanzania, jaji mkuu wa Zanzibar, manaibu spika, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wao watakuwa na taa za bluu-nyeupe-bluu na king’ora.

Ukiacha hao, mawaziri, matibu mkuu wa Serikali, Mwanasheria Mkuu (AG) na wengine wa hadhi hiyo msafara utakuwa na taa za bluu na sireni, wakati kwa Rais mstaafu msafara utakuwa na king’ora na taa za ukungu tu bila taa zinazong’ara.

Kwa wageni wa nchi za nje, kanuni hizo zinaeleza matumizi ya ving’ora na taa kwa wageni wa ngazi za juu kutoka nje yataamuliwa na waziri anayehusika na usafiri kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na vyombo vya usalama.

Matumizi ya ving’ora, filimbi au taa zinazomulika za magari ya dharura yaliyoidhinishwa yatakuwa ni magari au pikipiki za polisi zinazoweza kufungwa mchanganyiko wa taa zinazomulika, ving’ora au filimbi kulingana na mahitaji kutegemea aina ya msafara au hali ya dharura.

Kulingana na kanuni hizo, magari ya jeshi au vikosi vya ulinzi wakati wa dharura, yanaweza kufungwa taa zinazomulika za rangi nyekundu na bluu pamoja na ving’ora kulingana na aina ya dharura.

Kwa magari ya wagonjwa ya zimamoto au magari mengine ya dharura yaliyoidhinishwa yanaweza kufungwa taa za duara zinazomulika zenye ishara nyekundu na ving’ora kwa kutegemeana na aina ya dharura.

Kifungu cha saba cha kanuni hizo kinaeleza hairuhusiwi kuweka king’ora, kifaa cha kutoa ishara ya sauti, filimbi au taa ya tahadhari inayomulika kwenye gari au pikipiki, isipokuwa kama kuna idhini chini ya kanuni hizo, kibali ni kutoka kwa waziri.

Kanuni katika kifungu cha nane kinaeleza mtu anayekusudia kufunga ving’ora, kifaa cha kutoa ishara ya sauti, filimbi au taa ya tahadhari inayomulika, atatuma maombi ya kibali kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa njia ya barua.

Kifungu cha tisa kinaeleza mtu yeyote atakayefunga king’ora au vimulimuli wakati hajatajwa na sheria au bila kupata kibali cha waziri anatenda kosa la jinai na akitiwa hatiani atatozwa faini isiypungua Sh50,000 na isiyozidi Sh300,000.

Lakini sheria hiyo inaeleza endapo atashindwa kulipa faini hiyo, anaweza kufungwa kifungo ambacho si chini ya miezi sita lakini katika kutoa adhabu hiyo, kifungo atakachopewa hakitazidi miaka mitatu au adhabu zote kwa pamoja

Related Posts