Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila ametoa muda wa wiki mbili kwa uongozi wa Wafanyabiashara wadogo (Machinga) eneo la kariakoo kuanza kufungua njia ili kuruhusu magari kupita na shughuli za kibiashara kufanyika kwa ufanisi wakati Serikali ikielekea kufanya uzinduzi wa soko jipya la Kariakoo.
Akiongea Jijini Dar es salaam leo May 30,2025, RC Chalamila amesema kuelekea uzinduzi wa soko jipya ni muhimu kwa Machinga Kariakoo kufungua njia za kuingia ili kupeleka bidhaa kwenye soko jipya kwani soko hilo limeshakamilika kwa 98%.
RC Chalamila amesema Machinga watakaoondoshwa kwenye njia hizo zinazopaswa kufunguliwa watapelekwa kwenye maeneo maalum yanayotengwa kwani Serikali inatambua uwepo wao kwenye eneo hilo kama ambavyo Wizara ya TAMISEMI imeshaelekeza.
Kwa upande wake Meneja Mkuu Shirika la Masoko Kariakoo Ashrafu Abdulkarim amesema Shirika hilo linaendelea kuratibu Wafanyabiashara waliokuwepo kurejea kwenye soko hilo ambapo kwa idadi walikuwa 1520 lakini hadi sasa waliojisajili kwenye mfumo na kujaza fomu ni 1159 na kusema kuwa maeneo mengine ya wazi yaliyobaki yatatangazwa kupitia mfumo wa TAUSI ili yapate Wapangaji.
