Nature

Larry Madowo; Tulichoandika Kuhusu Tanzania Tupo Tayari Kudhibitisha

Kituo cha habari cha CNN kimesisitiza kuwa ripoti yake kuhusu matukio ya Oktoba 29, 2025 nchini Tanzania imejengwa kikamilifu juu ya ushahidi likibainisha kuwa hakikuchapisha taarifa yoyote ambayo halikuweza kuithibitisha.

Akizungumza na SABC News, mwandishi wa habari wa CNN, Larry Madowo alisema uchunguzi wao ulifanywa kwa kutumia mahojiano na zaidi ya Watanzania 100, uchambuzi wa kitaalamu wa sauti, ulinganifu wa video, na picha za satelaiti ili kufuatilia matukio ya vurugu, vifo na madai ya makaburi ya pamoja.

“Tulifanya kazi kwa umakini mkubwa. Tulihakiki kila ushahidi tulioupata na hatukutohoa taarifa yoyote bila kuwa na uthibitisho wake. Tuliikagua kila video na kila sauti, na ushahidi unaonesha wazi kuwa raia wasiokuwa na silaha walipigwa risasi na polisi au watu waliokuwa na bunduki,” alisema.

Alisema hakuna mtu wala mamlaka yoyote iliyokanusha ukweli wa taarifa zao tangu ziwekwe hadharani: “Tangu tulipotangaza ripoti hii, hakuna yeyote aliyesema kuwa tulidanganya au tuliandika taarifa za uongo.”

Wakati CNN ikisema imetekeleza uchunguzi wa kina, Serikali ya Tanzania kupitia Msemaji Mkuu wake Gerson Msigwa imepinga ripoti hiyo, ikieleza kuwa ina makosa ya kiweledi na imeegemea upande mmoja.

Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa juma, Msigwa alisema uhakiki wa maudhui ya CNN unaendelea lakini akasisitiza kuwa shirika hilo “halikutoa nafasi sawa kwa upande wa serikali.” Amesema mwandishi wa CNN hakuwasiliana na mamlaka za Tanzania na alitumia picha za simu bila kuzingatia taratibu za kiweledi.

“Hawakufuata maadili. Uandishi wa habari unatakiwa kuwa wa pande zote. Hatusemei vifo vilivyotokea; sote tumesikitishwa. Lakini kwa nini kutengeneza maudhui yanayoongeza maumivu na hasira kwa wananchi?” Alihoji Msigwa na kuongeza,

“Ni kinyume cha maadili kuchapisha picha mbaya ambazo hazijathibitishwa ipasavyo. Tume imeundwa kuchunguza na itatoa ripoti. Tunatoa wito CNN waje upande wa serikali wasikilize, na wachapishe taarifa zenye uwiano na ukweli.”

Related Posts