
Mchezaji wa Simba SC, Ibrahim Doumbia, amesema ameguswa sana na upendo na sapoti aliyopewa na mashabiki wa timu hiyo baada ya kushuka kwenye basi na kukutana na bango lenye ujumbe “WE ARE TOGETHER DOUMBIA. WE LOVE YOU.”
Doumbia amesema tukio hilo lilimgusa kiasi cha kumfanya kutokwa na machozi, akieleza kuwa katika soka kuna nyakati ngumu, ushindi, vipigo, lawama na wakati mwingine mashaka, lakini mashabiki wa Simba wamemkumbusha jambo moja muhimu kuwa hayuko peke yake.
Amesema mashabiki wote wa Simba tayari wana nafasi kubwa moyoni mwake na amewahakikishia kuwa ataendelea kufanya kazi kwa bidii, kupambana na kutoa kila alicho nacho kwa ajili ya jezi ya Simba.
“Nyakati hizi ngumu, In Shaa Allah, tutazishinda pamoja. Familia haitelekezi kila mmoja wakati wa changamoto. Familia hubaki pamoja, huinuka na kusonga mbele pamoja.”
Doumbia pia amewashukuru mashabiki wa Simba kutoka Tanzania nzima, wakiwemo wanaomhimiza, wanaomuombea, wanaomuamini pamoja na wanaomkosoa, akisema anawapenda wote na maoni yao yanampa nguvu zaidi ya kufanya kazi kwa bidii na kuwa bora.
Amesema hataki kuzungumza sana, bali anataka kufanya kazi, kujifunza, kuboresha uwezo wake, kupambana na muhimu zaidi kulipa upendo wa mashabiki kwa kiwango kizuri uwanjani.
“Nyakati bora bado zinakuja, In Shaa Allah. Asanteni kwa kila kitu, familia yangu ya Simba. Asanteni kwa upendo wenu, uvumilivu wenu na sapoti yenu. NAWAPENDA NYOTE. Simba Nguvu Moja!”
ALSO READ | Huyu Ndio Ng’wanamalundi Msukuma Aliye Washangaza Wakoloni wa Kijerumani kwa Nguvu za Giza


