
Hapana shaka, nguvu ya fedha ndio inaonekana imemshawishi nyota za zamani wa Yanga, Fiston Mayele, kuhamia Al Ahli Tripoli ya Libya katika dirisha kubwa la usajili linaloendelea akitokea Pyramids FC ya Misri.
Inaripotiwa kwamba timu hiyo ya Libya itamlipa mshahara wa Dola 5 milioni (Sh13.3 bilioni) katika kipindi cha miaka miwili ya mkataba wake
Katika kila mwaka wa mkataba wake, Mayele atavuna kiasi cha Dola 2.5 milioni (Sh6.6 bilioni).
Mayele amejiunga na Al Ahli Tripoli akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Pyramids FC.
Mchezaji9 huyo raia wa DR Congo amesema kuwa mipango mizuri ya klabu hiyo ndio imemshawishi ajiunge nayo.
“Kwanza kabisa, ninafurahi sana kuwa hapa. Nadhani nimepokelewa vizuri.
“Watu wengi wananiuliza kwa nini nilichagua Al-Ahli Tripoli. Kwa kweli, huo ndio uamuzi niliofanya. Pia ninaiona dhamira ya klabu.
“Rais ameweka juhudi kubwa sana. Ameleta wachezaji wazuri sana. Anataka timu yake iendelee kusonga mbele ili waweze pia kushinda mataji,” amesema Mayele.
Akiwa na Pyramids FC, Mayele alishinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, taji la Africa-Asia-Pacific, taji la ACF Super Cup, ubingwa wa Ligi Kuu Misri na amechukua mara moha kiatu cha dhahabu cha Ufungaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mayele ni miongoni mwa wachezaji watano waliosajiliwa na Al Ahli Tripoli katika dirisha hili kubwa la usajili la majira ya kiangazi, wengine wanne wakiwa ni Fagrie Lakay, Mostafa Sakshak, Hocine Dehiri na Mohammed Khalil
